March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yagusa afya Iringa,yatoa mashuka 455 hospitali ya rufaa

*Msaada huo kutatua upungufu wa mashuka katika hospitali za Mkoa wa Iringa

*EWURA  yasisitiza kuendelea kusaidia jamii

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Iringa

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),imetoa msaada wa mashuka 455,hospitali ya Rufaa ya Mkoa  Iringa,ili kuboresha huduma za kimatibabu hospitalini hapo.

Msaada huo  umetolewa Februari 10, 2026,  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Baraza la Wafanyakazi wa mamlaka hiyo, lililofanyika mkoani humo Februari 9 na 10,mwaka huu.

Akiwasilisha msaada huo Meneja wa EWURA Kanda ya Kati, Mhandisi Hawa Lweno,amesema mamlaka hiyo itaendelea na utaratibu wa kutoa mchango kwa jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo afya.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dkt. Alfred Mwakalebela,amesema msaada huo  utapunguza changamoto  ya upungufu wa mashuka, kwani kwa siku mgonjwa anatakiwa kutumia mashuka 6 lakini kwa sasa huduma hiyo haitoshelezi kutekeleza takwa hilo kwa kila mgonjwa.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa,Nuru Siyovelwa, alipokea msaada huo,amesema mashuka yamekuwa hayatoshelezi katika hospitali za Mkoa huo, hivyo ameishukuru EWURA kwa kuguswa kwani yatasaidia kutoa huduma bora kwa wananchi.