March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ukusanyaji wa Taarifa na Hatari za Kutoa Taarifa Binafsi Mtandaoni

Mwandishi: Ismail Mayumba

Ukusanyaji wa taarifa ni mchakato wa kukusanya, kuchambua na kuelewa taarifa kuhusu mfumo, mtandao, shirika au mtumiaji lengwa, kwa lengo la kufahamu jinsi mfumo huo unavyofanya kazi, teknolojia zinazotumika, pamoja na mianya ya kiusalama inayoweza kuwepo. Katika zama za sasa, sehemu kubwa inayotumika kukusanya taarifa ni mitandao ya kijamii na tovuti mbalimbali. Mara nyingi watu hutoa taarifa zao binafsi ili kupata huduma fulani, au kwa kutojua madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutoa taarifa hizo.

Kila mtumiaji wa mitandao ya kijamii hupenda kujulikana na kuonekana kwenye majukwaa hayo. Wengine hutumia mitandao hiyo kutangaza biashara zao, kufanya biashara moja kwa moja, au kutumia akaunti zao kama jukwaa la wafanyabiashara wengine. Katika karne ya sasa, mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikubwa cha kipato kwa vijana wengi, ambapo huingiza fedha kupitia matangazo na ushirikiano wa kibiashara kwenye majukwaa hayo.

Aidha, utoaji wa taarifa binafsi umegeuka kuwa biashara yenyewe. Watu wengi huuza taarifa zao au simulizi za maisha yao kwa sababu jamii ina hamu ya kufahamu yanayoendelea katika maisha ya watu mashuhuri. Haya yote ni faida zinazotokana na kutoa taarifa binafsi mtandaoni. Faida kubwa zaidi ni kupata utambulisho; mtu anapotafutwa mtandaoni hupatikana kwa urahisi, hadi kufahamu anapoishi, jambo ambalo linaweza kusaidia kupata ajira au fursa nyingine za maendeleo.

Hata hivyo, wahenga walisema:
“Ukiacha dirisha wazi ili hewa ipite, ujue pia wadudu wataingia.”
Methali hii inaakisi uhalisia wa mitandao ya kijamii—faida huja sambamba na hatari.

Umashuhuri unapoongezeka mtandaoni, hasa kwa mtu mwenye hadhi ya kisiasa, kifedha au kijamii, huanza kuvutia watu wenye nia ovu. Wengine hujaribu kufaidika kwa kukuchafua, kukuibia mali zako, au kutumia taarifa zako vibaya. Kadri mtu anavyoweka taarifa nyingi mtandaoni au kushiriki kila hatua ya maisha yake hadharani, ndivyo wahalifu wanavyopata mwanya wa kumfahamu zaidi: kujua alipo, hali yake ya kifedha, na hata kupata picha au video ambazo zinaweza kumharibia heshima yake katika jamii.

Swali muhimu linalojitokeza ni:
Je, tunawezaje kutumia mitandao ya kijamii bila kutoa taarifa binafsi zinazoweza kutuhatarisha?

Baadhi ya taarifa ambazo si salama kuzitoa mtandaoni ni:

  • Taarifa za siri za kifedha
  • Nenosiri (passwords)
  • Anwani kamili ya makazi
  • Taarifa za safari na mahali ulipo kwa wakati halisi
  • Picha zenye taarifa nyeti
  • Taarifa za watoto

Hizi ni taarifa muhimu ambazo kusambazwa kwake kunaweza kusababisha hasara kubwa, kwani wahalifu wa mitandao wanaweza kuzitumia kwa manufaa yao binafsi.

Kwa hiyo, wakati mtu anapofurahia faida za kutoa taarifa zake binafsi mtandaoni, ni muhimu pia kuchukua tahadhari na kuweka mipaka. Uelewa wa hatari za mitandao ya kijamii na nidhamu ya matumizi yake ni silaha muhimu katika kujilinda dhidi ya wizi wa mitandaoni na matumizi mabaya ya taarifa binafsi.