Mwandishi: Ismail Mayumba
Katika matumizi ya kila siku ya WhatsApp, mara nyingi watumiaji hukutana na hali mbalimbali zinazoweza kuleta wasiwasi kuhusu usalama wa akaunti zao. Baadhi ya hali hizi huweza kumfanya mtumiaji ahisi kama amedukuliwa, au kama taarifa zake binafsi zinachukuliwa bila ridhaa yake. Wasiwasi huu hupelekea baadhi ya watu kusitisha mawasiliano na mtu fulani, kumzuia (block), kufuta namba yake, au hata kuacha kabisa kutumia mazungumzo hayo. Hata hivyo, hatua sahihi zaidi ni kutafuta ufafanuzi wa kitaalamu kabla ya kuchukua maamuzi, kwani si kila tukio lisilo la kawaida huwa ni hatari ya kiusalama.
Moja ya hali inayosababisha maswali mengi ni pale mtumiaji anapofungua mazungumzo binafsi (chat) au ya kikundi (group) na kuona ujumbe unaosema: “Your security code with +255 761 876 400 changed. Learn more.” Ujumbe huu huonekana kama onyo la kiusalama, lakini kwa uhalisia wake, hauashirii uwepo wa udukuzi au hatari ya moja kwa moja kwenye akaunti yako ya WhatsApp.
Kiufundi, ujumbe huu unatokana na mfumo wa usalama wa WhatsApp unaotumia teknolojia ya end-to-end encryption. Mfumo huu huhakikisha kuwa mawasiliano yako yanasomwa na wewe pamoja na unayewasiliana naye pekee. Pale kunapotokea mabadiliko fulani kwenye akaunti ya mtu unayechati naye, WhatsApp hubadilisha security code na kukujulisha ili kukuonyesha kuwa mazingira ya usalama yamebadilika.
Mabadiliko haya ya security code yanaweza kutokea endapo mtumiaji mwingine ameondoa WhatsApp kwenye simu yake kisha akaisakinisha tena, au kama amejiunga (login) kwenye kifaa kipya tofauti na kile alichokuwa akitumia awali. Vilevile, ujumbe huu unaweza kuonekana kama mtumiaji amebadilisha namba yake ya simu, ametoka (logout) kwenye kifaa kingine alichokuwa ametumia, au kama WhatsApp imefanya maboresho ya mipangilio ya encryption kwa ajili ya kuimarisha usalama.
Ni muhimu kufahamu kuwa katika mazingira haya yote, ujumbe huo ni wa taarifa tu na hauonyeshi kuwa mazungumzo yako yamesomwa na mtu mwingine au kuwa akaunti yako iko hatarini. WhatsApp hutumia ujumbe huu kama njia ya kukujuza mabadiliko ya kiufundi yanayohusiana na usalama wa mawasiliano.
Zaidi ya hayo, ni vyema kuimarisha usalama wa akaunti yako kwa kutumia hatua za ziada kama vile Two-Step Verification (2-Step Authentication). Hatua hii huongeza ulinzi wa akaunti yako hata kama mtu mwingine atajaribu kuifikia bila ruhusa. Kwa kufanya hivyo, utakuwa umeongeza kiwango cha usalama na kupunguza uwezekano wa matatizo yanayohusiana na uhalifu wa mtandaoni.
Kwa ujumla, ujumbe wa “Your security code changed” si tishio bali ni sehemu ya mifumo ya kawaida ya kiusalama ya WhatsApp. Ufahamu sahihi wa teknolojia hii hukusaidia kutumia mitandao ya kijamii kwa kujiamini zaidi na bila hofu isiyo ya lazima.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama