Na Joyce Kasiki, Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Subira Mgalu, amesema Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 imeleta matumaini mapya kwa wananchi wa Bagamoyo, hususan katika sekta ya viwanda, uwekezaji na miundombinu, akisema miradi iliyotajwa imeanza kuonyesha matokeo ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais katika kipindi cha pili cha Awamu ya Sita.
Akichangia hotuba hiyo bungeni jijini Dodoma, Mgalu alisema nia ya Rais ya kuanzisha kongani mpya ya viwanda katika Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo ni jambo lililosubiriwa kwa muda mrefu, takribani miaka 15, tangu eneo hilo lipimwe kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa viwanda.
Alieleza kuwa kwa mara ya kwanza, Desemba 30, 2025, wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo walishuhudia hatua ya kihistoria baada ya Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kufika wilayani humo akiwa na wawekezaji sita na kuwakabidhi hati za uwekezaji, kwa lengo la kujenga viwanda ndani ya mwaka mmoja.
Mbunge huyo aliongeza kuwa ndani ya siku 100 za utekelezaji wa Serikali, pia kumeonekana ushahidi wa kuanza kwa mradi wa ujenzi wa Bandari Mpya ya Bagamoyo, baada ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kwa ajili ya ujenzi wa gati tatu, hatua aliyoitaja kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.
Mgalu alisema miradi hiyo mikubwa yote imepelekwa rasmi katika Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, hatua inayothibitisha dhamira ya Serikali ya kuifanya Bagamoyo kuwa kitovu cha viwanda na biashara. Hata hivyo, aliomba Serikali iharakishe malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati.
Alibainisha kuwa tayari Serikali imeanza mchakato wa kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi katika maeneo ya Kondo, Mlingotini, Pande, Zinga, Tiseza na Kiromo, ambako ardhi imechukuliwa kwa ajili ya miradi hiyo.
“Licha ya kusubiri kwa muda mrefu, sasa tumeanza kuona dalili za utekelezaji. Kwa maelekezo ya Serikali katika hatua za awali, tuna imani wananchi watalipwa fidia stahiki na kupewa makazi mbadala,” alisema Mgalu.
Akizungumzia mustakabali wa maendeleo ya Bagamoyo, Mbunge huyo alisema ufuatiliaji wa karibu wa miradi mikubwa, ikiwemo ujenzi wa barabara ya Makofia–Mlandizi na kipande cha reli ya kisasa (SGR) kutoka Kwala hadi eneo la viwanda, unatoa picha ya mabadiliko makubwa yanayokuja.
Kwa mujibu wa Mgalu, ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, Bagamoyo inatarajiwa kubadilika kwa kasi na kuwa mji wa mfano kiuchumi, kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina