*Wazazi Mwanza waomba serikali kugharamia vifaa vya elimu kwa wanafunzi
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza
TAASISI ya The Desk & Chair Foundation,imeendelea kutoa msaada wa vifaa vya elimu kwa zaidi ya wanafunzi 500 wenye uhitaji wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza waendelee na masomo bila vikwazo.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Alhaji Dk. Sibtain Meghjee,amesema msaada huo ni endelevu na unalenga kuhakikisha wanafunzi wote wanaokosa vifaa muhimu vya shule hawapotezi fursa ya kupata elimu ambapo kwa miaka 10, taasisi hiyo imekuwa ikisaidia jamii na familia duni zisizo na uwezo wa kugharamia mahitaji ya shule kwa watoto wao.

Amesema awamu hiyo ni ya pili ya msaada wa mwaka mpya wa masomo 2026,imewahusisha wanafunzi zaidi ya 500 wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza huku awamu ya kwanza wanafunzi 1,000 walinufaika na msaada huo.
Kwa upande wake, Hamisi Kibugwa, mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Kakebe,amesema baada ya kufiwa na wazazi wake anaishi maisha ya dhiki pamoja na babu na bibi yake, hali inayowafanya washindwe kumudu mahitaji ya shule.
“Ili kupata fedha za kujikimu, babu na bibi walikuwa wakiuza udongo (pemba), lakini sasa hawana mtaji. Naiomba serikali iigharamie vifaa vya shule kwa wanafunzi wasio na uwezo baada ya kutambuliwa, ili tuondokane na changamoto ya kukosa vifaa vya elimu,”amesema na kuishukuru The Desk & Chair Foundation kwa msaada huo, ingawa mahitaji yake bado, ana uhitaji wa madaftari mengine saba.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutenga fedha au kutafuta vyanzo maalum vya kugharamia vifaa vya elimu, ili watoto waweze kupata elimu bila vikwazo.
Wamesema kuwa katika miaka ya 1970, elimu ilitolewa bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, ambapo wazazi waligharamia sare pekee, huku wanafunzi wakisafiri kwa hati maalum kwenda shule za sekondari na vyuo, kikiwemo chuo kikuu.
Hata hivyo, walieleza kuwa mabadiliko ya kiuchumi na utekelezaji wa sera za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) za miaka 1980, hususani kuanzia 1985 (Mpango wa Marekebisho ya Uchumi), ziliifanya serikali ijiondoe kugharamia elimu na huduma zingine za jamii kama afya bure
“Elimu ilikuwa bure kabisa isipokuwa sare za shule. Mpango wa usafiri kwa wanafunzi ulikuwepo, lakini ulifutwa baada ya mageuzi ya kiuchumi. Sera hizo zililenga kusaidia nchi zilizokuwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, ikiwemo Tanzania, kwa kutoa mikopo na misaada ya kifedha kwa masharti maalum,”amesema mmoja wa wazazi kwa hifadhi ya jina.
Ameeleza kuwa, miongoni mwa masharti hayo ilikuwa kupunguza matumizi ya Serikali katika huduma za jamii kama elimu na afya,kujiondoa kwa Serikali kugharamia huduma zote kikamilifi,kuhamasisha mchango wa wananchi katika huduma za kijamii
“Kutokana na masharti hayo, serikali ya Tanzania iliacha sera ya elimu bure ambayo awali iligharamia ada za shule,ununuzi wa vifaa vya elimu ( vitabu, madaftari na vifaa vya kufundishia),kulipia gharama nyingine za uendeshaji wa shule,”amesema mzazi huyo.

Ameongeza kuwa, badala yake, wazazi na walezi walianza kuchangia gharama za elimu, ikiwemo kununua vifaa vya shule na kulipa ada mbalimbali, hatua hiyo ililenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa serikali lakini ilisababisha kupungua kwa uandikishaji wa wanafunzi, hasa kutoka familia maskini.
Kuongezeka kwa tofauti za kielimu kati ya matajiri na maskini na kushuka kwa ubora wa elimu katika baadhi ya maeneo, hivyo sera za Benki ya Dunia na IMF za mwaka 1985 zilichangia kuondolewa kwa elimu bure nchini, zikiakisi mabadiliko ya sera za kiuchumi kutoka mfumo wa ujamaa kwenda uchumi wa soko huria.
Walisema pamoja na Serikali kufanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu, hususani katika ujenzi wa miundombinu, ipo haja ya kuangalia suala la vifaa vya elimu.
“Rai yangu serikali iangalie namna ya kugharamia vifaa vya elimu ili kuwaondolea watoto changamoto hiyo, wasome kwa kupata maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya jamii.Pia, niwashukuru The Desk & Chair Foundation kutoa vifaa vya elimu bure,mashirika na taasisi ziige kusaidia jamii ,”ameaema Alex Nyawambo, mkazi wa Kanyerere.
“Niipongeze taasisi ya The Desk & Chair Foundation, kwa kufadhili watoto wenye uhitaji waliopo shuleni, ni msaada mkubwa kwa watoto wa Kitanzania kuhakikisha wanapata elimu bila kikwazo,”amesema Tawfiq Ali, mkazi wa Isamilo .
Waliongeza kuwa serikali inaweza kutenga fedha za ruzuku ya vifaa vya elimu kama ilivyofanya kwa waagizaji wa mafuta, hatua itakayopunguza mzigo wa gharama za elimu kwa wazazi ambao ni walipa kodi wakubwa.



More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi