Na Mohammed Sharksy – SUZA
Kwa mtoto, kusikia si jambo dogo. Kusikia ni mlango wa kujifunza, kuwasiliana, kuelewa dunia inayomzunguka na kuunda mahusiano ya kijamii.
Pale mlango huu unapofungwa, maisha ya mtoto hubadilika kwa kiasi kikubwa. Hali hii imekuwa halisi kwa watoto wengi wa Zanzibar wanaokumbwa na magonjwa sugu ya masikio, hususani maambukizi ya masikio ya muda mrefu (otitis media), yanayosababisha kutokwa na usaha masikioni na kupungua kwa uwezo wa kusikia.

Hivi karibuni, matumaini mapya yamerudi kung’aa kwa watoto hawa baada ya Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo (ENT), Li Li, Mkurugenzi wa Kitengo cha Upasuaji wa Masikio kutoka Timu ya 35 ya Madaktari wa China walioko Zanzibar, kuzindua wiki maalum ya upasuaji wa masikio kwa watoto wenye otitis media.
Ambapo kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ya upasuaji wa masikio kwa kutumia kiotoscope (upasuaji mdogo usio na majeraha makubwa), watoto wengi waliokuwa wamepoteza matumaini ya kusikia walipata nafuu na kurejea katika ulimwengu wa sauti.
Zaidi ya matibabu, mpango huu umeimarisha urafiki wa kitabibu kati ya China na Tanzania (Zanzibar), na kuonesha uso wa ubinadamu wa taaluma ya udaktari,ambapo huruma, utaalamu na ushirikiano vinakutana kwa lengo la kuokoa maisha na mustakabali wa watoto.
Mizigo ya Kimya inayoathiri watoto
Zanzibar ina hali ya hewa joto na unyevunyevu karibu mwaka mzima pamoja na changamoto za miundombinu ya usafi katika baadhi ya maeneo.Mazingira haya yamechangia kuenea kwa maambukizi ya masikio kwa watoto hasa otitis media ya muda mrefu.
Watoto wengi hukosa matibabu ya mapema kutokana na ukosefu wa wataalamu wa masikio, uelewa mdogo wa jamii na uwezo mdogo wa kifedha wa familia. Matokeo yake ni watoto kuishi kwa miaka mingi wakiwa wanatokwa na usaha masikioni (otorrhea).
Pia maumivu ya masikio yanayojirudia,kupungua au kupoteza uwezo wa kusikia,kushindwa kufuatilia masomo darasani.Hata hivyo kupungua kwa uwezo wa kusikia hakuathiri masikio pekee bali huathiri maendeleo ya lugha, elimu, kujiamini na mahusiano ya kijamii.
Mara nyingi watoto hawa huonekana kama wasikivu au wasiozingatia masomo ilhali tatizo lao ni la kiafya.
Daktari Li Li na dira ya mabadiliko
Baada ya kuwasili Zanzibar, Daktari Li Li anatumia muda kufahamu changamoto za watoto wa Zanzibar katika afya ya masikio. Akiwa na uzoefu wa kikwango cha juu katika tiba na upasuaji wa masikio kwa njia zisizo na majeraha makubwa,ametambua kuwa watoto walihitaji mbinu salama, sahihi na rafiki kwa umri wao.
Masikio ya watoto yana muundo mdogo na dhaifu hivyo upasuaji wa kawaida wa kufungua kwa kiwango kikubwa unaweza kuleta majeraha makubwa, maumivu makali na muda mrefu wa kupona.
Kwa msingi huo, Daktari Li Li alianzisha mfumo wa uchunguzi na matibabu kwa kutumia kiotoscope, ambacho kinampa daktari uwezo wa kuona ndani ya sikio kwa uwazi na kufanya upasuaji mdogo kwa usahihi mkubwa.
Lengo la upasuaji huo ni kuondoa chanzo cha maambukizi bila kuharibu tishu salama,kupunguza maumivu na hatari kwa mtoto,kuharakisha kupona pamoja na
kuboresha uwezo wa kusikia kwa kiwango kikubwa.
Safari ya Hassan kurejea latika Dunia ya sauti
Miongoni mwa watoto waliopata matibabu katika wiki hiyo alikuwa Hassan (siyo jina halisi), mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 10,ambaye ameugua otitis media sugu kwa zaidi ya miaka mitano huku akitokwa na usaha mara kwa mara ambao umesababiaha kupungua uwezo wa kusikia.
Katika mazingira ya shule, Hassan alikuwa akipata shida kuelewa maelekezo ya walimu hivyo alikaa nyuma darasani, akijibu vibaya au kutokujibu maswali. Wakati mwingine alionekana kama mtoto mkaidi au mzembe, jambo lililomuumiza kihisia.
Baada ya uchunguzi wa kina na Daktari Li Li, ilibainika Hassan anahitaji upasuaji wa haraka ambao ulifanyika kwa kutumia teknolojia ya ‘otoscopic minimally invasive’, ambapo chale ndogo sana ilitumika kufanya utaratibu.
Matokeo yalikuwa ya kushangaza siku ya tatu baada ya upasuaji ambapo usaha ulikuwa umetoweka huku vipimo vya kusikia vilionesha kuboreka kwa kiwango kikubwa.
Hassan mwenyewe alithibitisha mabadiliko hayo kwa kufaraha ambapo anasema,”Sasa ninasikia sauti ya mwalimu vizuri,”.
Kwa Hassan, huu haukuwa upasuaji tu bali ulikuwa mwanzo mpya wa maisha ya elimu, mawasiliano na kujiamini.
Wiki ilioleta mabadiliko kwa watoto wengi
katika kipindi cha wiki ya upasuaji wa masikio, watoto wengi waliopata mateso ya muda mrefu walifanyiwa upasuaji kwa mafanikio makubwa.
Huku wazazi wakishuhudia watoto wao wakipona haraka bila maumivu makali na kurejea katika hali ya kawaida kwa muda mfupi.
Watoto wengi walikuwa wameishi kwa miaka wakiamini hali yao haiwezi kutibika dhana hiyo ilivunjwa na wiki hiyo na kuleta matumaini mapya kwa jamii nzima.

Daktari Li Li,anasisitiza kuwa teknolojia pekee haitoshi hivyo anasema,”Kilicho muhimu zaidi ni kuhakikisha maarifa hayo yanabaki hapa na yanatumika kuwatibu watoto wengi zaidi hata baada ya sisi kuondoka,”.
Moja ya nguzo kuu za mpango huu ilikuwa ni kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani kwa kuzingatia falsafa ya misaada ya kitabibu ya China ya “kufundisha kuvua samaki badala ya kumpa samaki”, Daktari Li Li aliwahusisha moja kwa moja madaktari na wahudumu wa afya wa Zanzibar.
Katika vyumba vya upasuaji:
Madaktari wa ndani walifundishwa matumizi ya kiotoscope,walijifunza mbinu za msingi za upasuaji wa masikio kwa watoto ambapo walishiriki hatua kwa hatua chini ya uangalizi wa karibu.
Hivyo mwisho mwa wiki, baadhi ya madaktari wa ndani waliweza kufanya utaratibu wa msingi kwa kujitegemea, jambo lililoweka msingi wa huduma endelevu za masikio kwa watoto katika hospitali za Zanzibar.
Afya Endelevu Badala ya Msaada wa Muda Mfupi
Tofauti na programu nyingi za misaada ya muda mfupi, mpango huu ulilenga uendelevu wa huduma za afya. Kupitia uhamishaji wa ujuzi na uzoefu:
Watoto wengi zaidi watapata matibabu karibu na makazi yao
Gharama za rufaa zitapungua
Ulemavu wa kudumu wa kusikia utapunguzwa kwa kiasi kikubwa
Taswira halisi ya misaada ya kitabibu ya China
Kazi ya Daktari Li Li ni mfano hai wa mpango wa misaada ya kitabibu wa China barani Afrika, ulioanzishwa kwa lengo la kusaidia nchi rafiki kuboresha mifumo yao ya afya.
Kwa miongo kadhaa, madaktari wa China wamekuwa wakivuka bahari na mabara wakibeba utaalamu, vifaa na moyo wa kujitolea.Zanzibar sasa inanufaika si tu na tiba pia na maarifa yatakayodumu kwa vizazi vijavyo.
Hatua kuelekea mustakabali wa afya ya pamoja
Magonjwa hayana mipaka, wala hayachagui taifa au rangi,kupitia kurejesha kusikia kwa watoto wa Zanzibar, Daktari Li Li na timu ya Madaktari wa China wameonesha maana halisi ya ushirikiano wa kimataifa katika afya.
Kwa taaluma, huruma na ushirikiano, wamegeuza dhana ya mustakabali wa pamoja wa afya ya binadamu kuwa uhalisia unaoonekana katika tabasamu la mtoto, sauti inayorejea na matumaini mapya ya maisha.
Watoto kama Hassan wanaporejea shuleni wakiwa wanasikia tena, sauti zao zinakuwa ushuhuda hai kwamba tiba yenye ubinadamu haisikiki tu masikioni, bali moyoni pia.


More Stories
Wanawake wa milimani waendelea kuumia licha ya ahadi za COP29
Taasisi nyingi,Serikali moja na misitu ya Kilimanjaro inayopotea
Ukusanyaji wa Taarifa na Hatari za Kutoa Taarifa Binafsi Mtandaoni