March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania waepuke kushabikia vitendo vya uvunjifu wa amani

Na Agnes Alcardo

AMANI ni hali ya utulivu,usalama na kutokuwepo kwa migogoro au vurugu hii ikiwa na maana ya watu kuishi kwa kuelewana,kuheshimiana na kutatua tofauti bila kutumia nguvu.Pia inaweza kurejelea utulivu wa ndani wa mtu yaani kuwa na moyo na mawazo tulivu bila ya wasiwasi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye amani, nchi ambayo tangu awali ilijiwekea misingi ya utulivu, amani, umoja, mshikamano na upendo kwa watu wake.

Ikumbukwe kuwa, endapo amani ikitoweka ni vigumu kuirudisha na kuwa hali kama ya awali, badala yake ni vyema kila mmoja akailinda kwa kuhubiri juu ya amani, mshikamano na kila mmoja kuwa mzalendo hususani kwa taifa lake.

Hivi karibuni kumejitokeza vitendo vya kujaribu kuiharibu amani ya nchi, amani ambayo ilihasisiwa na watangulizi wa Taifa la akiwepo Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, ambaye kwa hali na mali alihakikisha nchi inakuwa huru chini ya kivuli cha amani, umoja na mshikamano.

Hali ya sintofahamu ilizuka Oktoba 29, 2025 siku iliyokuwa ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, ambayo ilimtaka kila mtanzania aliyekuwa na vigezo vya kupiga kura, kuitumia siku hiyo kutimiza haki yake ya msingi ya kuchagua wagombea anaowataka kwa nafasi ya Urais, wabunge na madiwani watakao ongoza kwa kipindi cha miaka mitano 2025-2030.

Mapema siku hiyo baadhi ya vikundi vya vya vijana ‘Gen z’ walijitokeza barabarani kwa yale waliyodai kuwa ni maandamano, ambapo baada ya muda mfupi hali ilibadilika na kupelekea baadhi ya watu kupoteza maisha, kupata majeraha na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Vitendo vya maandamano hayo yaliyosababisha vurugu nchini, kumeleta madhara kwa watu wengi, ambao waliandamana na wasiyo andamana wakati na baada ya maandamano hayo.

MAONI YA WANANCHI KUHUSU MAANDAMANO

Gazeti la Majira limefanya mahojino na watu mbalimbali kusikia wanaeleza nini kuhusu maandamano hayo, ambapo wengi wao wameonekana kukemea vitendo hivyo wakieleza kuwa vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo yao.

Mussa Kanuti (36) mkazi wa Dar-es-Salaam, ambaye anajishughulisha na biashara ya mbogamboga na viungo katika Soko la Ilala, anasema, kutokana na vurugu zilizosababishwa na maandamano, zilisababisha kushindwa kutoka ndani kwenda katika shughuli zake.

Anasema, ilimlazimu kukaa ndani kwa siku tatu akihofia uhai wake hali iliyomsababishia kushuka kiuchumi na kumletea ugumu wa kuhudumia familia yake.

“Nakemea vitendo vilivyojitokeza Oktoba 29,2025, vurugu zilizosababishwa na maandamano zilituathiri wengi hata ambao hatukushiriki kuandamana, nilisimamisha shughuli zangu mpaka nilipoona hali imetulia. Hivyo niliyumba kidogo kwenye kuhudumia familia yangu kutokana na kutoingiza tena kipato,”anasema Kanuti.

Vincent Mushi (40), mkazi wa Dar-es -Salaam, ofisa ushafirishaji (bodaboda)anasema hali ilikuwa siyo nzuri hususani kwao bodaboda.

“Sisi tunapotoka ndiyo tunapata fedha ya kula na ya bosi, sasa kwa vurugu kama zile inaturudisha wengine nyuma kwani mazingira yetu ya kujipatia kipato yanakuwa magumu, lakini tunashukuru Jeshi la Polisi kwa kuimarisha ulinzi,”anasema Mushi.

Nao baadhi ya Mama lishe walionekana kukemea vitendo vya kuhamasisha maandamano na kudai kuwa, vitendo hivyo vinavunja amani na kukwamisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aisha Maduu (46) mkazi wa Dar-es-Salaam, ambaye anajishughulisha na shughuli za mama lishe maeneo ya Vingunguti,amewataka watanzania kuwa wazalendo kwa nchi yao na kuachana na vitendo vya kuhamasisha vurugu badala yake kujishughulisha na shughuli mbalimbali ili kujiingizia kipato na kuwa na unafuu wa maisha.

“Si vyema sisi kama watanzania wazalendo tukawa mstari wa mbele kujihusisha na vitendo vya maandamano ambayo hapo.Awali hatukuwa nayo katika nchi yetu,tusiwasikilize wachache wanaotuchochea kwenye mitandao kwa lengo la kuharibu nchi yetu kwani tukifanya hivyo madhara yake ni makubwa,”anasema Aisha.

Kwa mfano kwa yale maandamano ya Oktoba 29, yamedhuru watu wengi kwa namna mbalimbali.

“Mimi ninayefanya kazi ya mama lishe sikupika karibu siku mbili,ninaishi kwa kutegemea biashara hiyo, Nina watoto watatu na wote wananitegemea lakini kwa siku zile mbili ambazo sikupika maana yake sikuingiza kipato hivyo hali ya maisha ya mimi na wanangu ilikuwa siyo nzuri,”anasema Aisha.

Prisca Macha (30), muajiriwa kwenye moja ya kampuni jijini Dar-es +Salaam,anasema, vitendo vya maandamano vimeleta ugumu katika maeneo mbalimbali na kuwasababishia watu kufanya kazi katika mazingira tofauti na awali, lakini pia kutokuwepo kwa usafiri wa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Anaiomba Serikali kuendelea kuimarisha ulinzi na kukemea vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

“Mimi ninafanya kazi (anataja), baada ya vurugu za maandamano watu wote ofisini tuliambiwa tusiingie hivyo hatukuingia, lakini hata baada ya kurudi tena kazini tulipata tabu sana kwani hata usafiri haukuwepo na gharama iliongezeka.Pia tulikuwa na mashaka juu ya usalama wetu, lakini tunashukuru kwa ulinzi kuimarishwa na tunaomba Serikali iendelee kuimarisha ulinzi hivi hivi,”anasema Prisca.

Sambamba na shuhuda hizo, pia wapo waliopata majeraha wakati wa vurugu zilizotokea kwenye maandamano Oktoba 29, 2025 na wengine waliopoteza ndugu zao kufuatia vurugu hizo.

Amos Barton (22) ameelezea jinsi alivyopata jeraha katika mguu wake wa kushoto, wakati aliposhiriki kwenye maandamano hayo.

“Kiukweli sitaki kusikia tena kitu maandamano,kwa namna moja yamenisababishia ulemavu wa mguu kama unavyoniona siwezi kutembea vizuri ninachechemea,”anasema Barton.

Nae Carolin Mwasandube,anaeleza kuwa maandamano hayo yamekuwa chanzo cha kifo cha ndugu yake, huku akiwataka watanzania hususani vijana kutojiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani kwani matokeo ya madhara yanayowapata ni huzuni kwa familia zao.

NINI KIFANYIKE?

Ipo haja ya kila mwananchi kuwa mzalendo kwa nchi yake, kulipenda, kuhubiri juu ya amani, mshikamano na upendo na kutokuwa chanzo cha uvunjifu wa amani nchini.

Ni vyema kutumia 4r (maridhiano) za Rais wa Jamhuri ya Muungano a Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mambo mbalimbali na si kwa njia nyingine zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Si busara kuwaunga mkono wachache wanaotaka kuwepo na uvunjifu wa amani wakitumia vigezo vya udini hali ambayo inaweza kusababisha machafuko kwa Taifa kama ambavyo hivi karibuni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwenye moja ya hotuba zake alipokemea vitendo vya kuvunja amani kwa kutumia dini na kuwataka viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kuhubiri amani.

Ni vyema kudumisha amani kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo kwani nchi pekee ya vizazi hivyo ni Tanzania. Lakini pia kuunga mkono juhudi za Serikali kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.