March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazalishaji wa batiki Dar wanufaika na mafunzo ya OSHA 

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar

WANAWAKE zaidi ya 200 wanaojihusisha na utengenezaji wa bidhaa za batiki wamenufaika na mafunzo ya usalama na afya yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya shughuli zao kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya mahali pakazi.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyogharamiwa na Serikali yametolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pakazi (OSHA) katika eneo la Ilala jijini Dar-es-Salaam.

Akifungua mafunzo hayo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira na Mahusiano,Rahma Kisuo,amewataka OSHA kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu kwani ni muhimu kwa wajasiriamali wadogo.

“Wajasiriamali wadogo ni kundi muhimu na lenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa letu,hivyo ni muhimu kuwapatia mafunzo ili waweze kutekeleza shughuli zao katika hali ya usalama,” amesema Kisuo.

Pia amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza ajali,magonjwa na vitendo vinavyoweza kutokea kutokana na ukosefu wa mifumo ya usalama na afya ikiwemo wafanyakazi wenye uelewa wa masuala husika.

Audha ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kutojihusisha na makundi yenye nia ya kuvuruga shughuli za uzalishaji na kuvunja amani ya nchi ya Tanzania.

Awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa utekelezaji wa program ya afya yangu,mtaji wangu ili kuziba mwanya wa uelewa wa masuala ya usalama na afya uliopo baina ya sekta rasmi na isiyo rasmi.

“Kupitia program hii tumekuwa tukiainisha makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo na kuwawezesha kwa mafunzo pamoja na kuwapatia vifaa kinga muhimu kutegemeana na aina ya shughuli zao,”amesema Mwenda.

Amesema program hiyo itaendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali hususani vijana, ambao kwa mujibu wa tafiti za  OSHA za hivi karibuni ndio waathirika wakubwa wa ajali katika maeneo ya uzalishaji kutokana na uelewa mdogo na ukosefu wa uzoefu kazini.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ,Jesca Charles, ameishukuru OSHA kwa kuwapatia elimu na vifaa kinga ambavyo vitawasaidia kujikinga dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa hususani kemikali ambacho ndio kihatarishi kikubwa katika uzalishaji wa bidhaa za batiki.