Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo ofisi ya DPP kuchuja makosa ya vijana wanaoshtakiwa kwa makosa ya uhaini kufuatia maandamano yaliozaa vurugu wakati wa uchaguzi ya Oktoba 29,2025 na kwa wale waliofanya makosa kwa kufuata mkumbo waachiwe huru.
Dkt.Samia amezungumza hayo Novemba 14,2025 akifungua na kuhutubia Bunge la 13, jijini Dodoma,ambapo kabla ya kuanza hotuba yake ametumia dakika 1 kwa ajili ya kuwakumbuka wale wote walipoteza maisha katika vurugu hizo huku akitoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao na waathirika wa vurugu hizo.
“Natambua kuna Vijana wengi wamekamatwa kwa kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya na wengine wamefuata mkumbo, nikiwa kama Mama navielekeza vyombo vya kisheria kuangalia makosa yaliyofanywa na vijana wetu, kwa wale ambao walifanya mambo kwa kufuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao,”amesema Dkt.Samia na kuongeza:
“Ukiangalia ‘clip’ zile za maandamano unaona kabisa kuna vijana waliingia kwa kufuta mkumbo, wanaimba kwa ushabiki, naelekeza Ofisi ya DPP kuchuja viwango vya makosa na kwa waliofuata mkumbo wawaachie waende kwa wazazi wao,”.
Hata hivyo Dkt.Samia ametumia maandiko matakatifu wakati wa kuagiza vyombo hivyo kwa kunukuu kifungu kutoka kitabu cha Luka 23:34 isemayo,”Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo”.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi