November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee Magu waahidi kura kwa Dkt. Magufuli

Na Daud Magesa, TimesMajira Online, Magu

WAZEE wa kata mbalimbali Wilayani Magu wameahidi kumpigia kura za heshima mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli kutokana na kazi kubwa alizofanya katika kukuza maendeleo.

Wazee hao wamesema, hawatapotea njia wala kudanganyika na sera za vyama vya siasa visivyoaminika ili kuonyesha ukomavu wa CCM wa kuleta maendeleo watampigia kura Dkt. Magufuli, wabunge na madiwani kwenye Jimbo la Magu.

Ahadi ya wazee hao ilitolewa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, baada na kuzungumza na wazee wa Kata za Jinjimili, Kabila,Gh’haya, Nkungulu katika Tarafa ya Ndagalu.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake, Thabitha Yakob mkazi wa Kijiji cha Mwashepi, amesema Dkt. Magufuli amewafanyia mengi yakiwemo ya ujenzi wa vituo vya afya na hospitali hivyo Oktoba 28, mwaka huu hawatamuangusha.

“Kwa aliyotufanyia Rais Magufuli hatukustahili kufanya uchaguzi lakini kwa kuwa ni utaratibu tunaomba aendelee kuongoza kwa miaka mingi na kwa kuthibitisha hilo Oktoba 28, tutampigia kura za kishindo yeye mbunge na madiwani kazi alizofanya ni kubwa,” amesema Yakob.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli akiteta jambo na Mzee Katemi Choluba wakati wa ziara yake ya kuzungumza na wazee wa kata mbalimbali wilayani humo.

Evarist Didas amesema, wanampongeza Mkuu wa Wilaya kwa uchapakazi, ukaribu wake kwa wananchi na kuwa hawajawahi kuona DC anayehangaika vijijini kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua

“Ni kiongozi wa mfano ingawa wamepita wengi Magu yeye amewapita, kwa muda mfupi ametembelea vijiji vyote 82 na kata 25, kila mara yuko vijijini kuwasilikiza wananchi, hajifungii ofisini hivyo Watanzania wampigie kura za ndiyo aendelee kuwatumikia wanyonge,” amesema Didas.

Kwa upande wake Kalli amesema, wazee ni lulu ya Taifa, wanastahili heshima na kuthaminiwa ili waendelee kupata heshima hiyo Oktoba 28, wasipotee bali wamchague Dkt. Magufuli anayeishi na shida za wazee na kuzitatua ili waishi kwa usalama na kunufaika kwa rasilimali za nchi na kufaidi matunda ya uhuru walioupigania.

Amesema, maendeleo yote yanayoonekana yameletwa na serikali ya CCM chini ya chini ya Rais Mafuguli, anajenga reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Nyerere la kufua umeme, Daraja la Kigongo-Busisi na pia barabara za Magu-Mahaha-Shishani hadi Bariadi na barabara ya Magu-Kwimba zitajengwa kwa kiwango cha lami, zote ziko kwenye ilani ya CCM.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, akizungumza na wazee wa Kata ya Nkungulu Tarafa ya Ndagalu

“Anafahamu jinsi wazee mlivyohaingaika kupigania uhuru wa Taifa hili, asitokee mtu wa kuwazunguka, wengine wanaomtukana hakuna walichowahi kukifanya cha maendeleo ,hivyo maendeleo hayo mmeyawezesha ninyi wazee, vijana hawakuwepo na hawajui uchungu wa nchi hii mliona nao hivyo msigawanyike muwezesheni Rais Magufuli kupata kura za kishindo,” amesema Kalli.

Akizungumzia mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) amesema kuwa, baada ya uchaguzi mkuu, wataalamu watapita kwenye vijijini vyote kuwabaini wanufaika waliosahaulika na kuingizwa kwenye mpango huo.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Magu pia ametoa msamaha kwa wazee wenye miaka zaidi ya 60 watakaofiwa na wenzi wao wakiwa wamelazwa hospitali ama vituo vya afya, wasitozwe gharama za kuhifadhi miili ya marehemu atalipa gharama hizo yeye (mkuu wa wilaya) na kusistiza wazee wataendelea kutibiwa bure na kuonya watumishi wa afya wanaowakejeli na kuwatolea lugha chafu, waaeche tabia hiyo.