Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benjamin Chiseo,amewaomba watanzania hususani vijana, kuendelea kuwa wazalengo kwa nchi yao kwa kulinda amani, upendo na umoja, huku akiwasisitiza kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa utulivu Oktoba 29, 2025.
Chiseo, ameyasema hayo Oktoba 26, mwaka huu, mkoani Mwanza, alipokuwa akiongea na vyombo vya habari, akiunga mkono juhudi za viongozi mbalimbali ambao wamekuwa wakisisitiza juu ya amani na kuwahasa kutowasikiliza wachache wenye nia ovu ya kuharibu amani ya nchi.
Amesema, kulinda amani ni jukumu la kila mtanzania, ili kuendelea kupata miradi mbalimbali ya maendeleo, akitolea mfano baadhi ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika sekta ya afya,elimu,kilimo,miundombinu ya barabara na sekta nyingine.
“Kwa ujumla nchi yetu ni nzuri sana hivyo tunatakiwa kuilinda kwa wivu mkubwa, hivyo niwaase watanzania wote hususani vijana wenzangu hakuna mafanikio bila amani na utulivu.Kwenye amani na utulivu tunapanga mipango mbalimbali kwa maendeleo ya nchi na maisha yetu kwa ujumla,”amesema na kuongeza:
“Tuwapuuze wale wachache wenye nia ovu ya kutaka tuungane kwa ajili ya kuvunja amani ya nchi yetu, nchi yetu ipo kwenye mikono salama chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo sisi kama vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa ni vyema tukawa mbele kuendelea kuhubiri juu ya amani kama ambavyo tumekuwa tukisikia maeneo mbalimbali hata kwenye mikutano ya mgombea Mwenza wa kiti cha Urais kupitia CCM Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi,tumekuwa tukisikia akihubiri juu ya amani, mshikamano na usalama wa nchi,”.
Aidha, amewahasa vijana kujishughulisha na shughuli mbalimbali ili kuweza kujipatia kipato, akielea uzuri wa maisha kwa kila mmoja hutokana na kujituma kwake na si vinginevyo.
“Vijana wenzangu siku zote mafanikio ni mchakato, hivyo ni vyema tukajituma kwa kufanya shughuli mbalimbali za kutuingizia kipato kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na si kulalamika tu,”amesema Chiseo

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako