March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekta ya Posta ina nafasi ya kukuza uchumi wa kidijitali

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholas Mkapa, amesema kuwa sekta ya Posta ina nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa kidijitali na inapaswa kuendelea kuwa jukwaa la ubunifu, ujumuishi na maendeleo ya kiteknolojia nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani, Mkapa amesema kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Posta kwa Ajili ya Watu: Huduma za Kizawa, Ufikaji Kimataifa”, inaakisi dhamira ya kuiendeleza sekta hiyo kuwa kiungo kati ya jamii na fursa za kiuchumi kitaifa na kimataifa.

“Sekta ya Posta imepitia mageuzi makubwa kutoka kuwa mtoa huduma za barua hadi kuwa mhimili wa biashara mtandao, usafirishaji wa bidhaa na miamala ya kidijitali. Hii ni ishara tosha kuwa mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi haupingiki,” amesema Mkapa.

Amesema Serikali inafurahia kuona jinsi Shirika la Posta Tanzania na wadau wengine walivyokumbatia mageuzi hayo kwa kuwekeza katika TEHAMA, kuboresha huduma na kuongeza ubunifu unaojibu mahitaji ya dunia ya sasa.

Katika maadhimisho hayo, washindi wa mashindano ya Uandishi wa Barua Kimataifa kwa Watoto pamoja na mashindano ya Ubunifu wa Mifumo ya Usafirishaji wa Huduma za Posta walitunukiwa zawadi mbalimbali.

Mashindano hayo yaliandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari, amesema maadhimisho ya mwaka huu ni fursa ya kuonesha namna ubunifu na uvumbuzi unavyoweza kuboresha huduma za posta katika zama za uchumi wa kidijitali.

“Lengo letu ni kuendeleza ubunifu ili kuweza kuboresha zaidi huduma za posta. Bila huduma za posta, hatuwezi kufika mbali,” amesema Dkt. Bakari.

Akizungumza kwa niaba ya Postamasta Mkuu, Mwakilishi wa Shirika la Posta, Arubee Ngaruka, all maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani, ambayo hufanyika kila Oktoba 9, ni jukwaa la kuonesha mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ngaruka amebainisha kuwa kwa sasa Shirika la Posta limeanzisha duka mtandao ambalo linawawezesha wafanyabiashara zaidi ya 1,000 kutoka Tanzania kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi kupitia mfumo wa kidijitali.

“Posta Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) wenye nchi wanachama 192. Hii ina maana kuwa bidhaa zinazowekwa kwenye duka letu mtandaoni zinaweza kuonekana katika nchi zote hizo,” amesema

Ameongeza kuwa jukwaa hilo limekuwa mkombozi mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao sasa wanaweza kuuza bidhaa zao kimataifa bila kupitia gharama kubwa au taratibu ngumu za usafirishaji wa jadi.