Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete,amesema ameridhishwa na maandalizi ya sherehe za kuhitimisha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, zitakazofanyika Oktoba 14, 2025, katika Uwanja wa Sokoine, mkoani Mbeya.
Akizungumza leo Oktoba 9, 2025, wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Waziri Kikwete amesema kuwa ameridhishwa na hamasa ya wananchi pamoja na nidhamu ya wakimbiza Mwenge.
“Moja ya sababu zilizonifanya nifike hapa ni kushuhudia afya na ari ya vijana wanaoukimbiza Mwenge wa Uhuru, pamoja na kuona hamasa ya wananchi wa Jiji la Mbeya katika kuukimbiza Mwenge huu wa kitaifa,” amesema Kikwete.
Aidha, amempongeza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, kwa uongozi na juhudi kubwa za kuhakikisha ujumbe wa Mwenge wa Uhuru unawafikia Watanzania katika maeneo yote ya nchi.

“Ni jambo la kujivunia kuona kuwa safari hii ya Mwenge imeendelea vizuri bila matukio mabaya. Kama Wizara, tunafarijika kwa kuona vijana wetu wanaonesha utii, uzalendo na ukakamavu — sifa kuu za kijana wa Kitanzania,” ameongeza liongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amepokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali na kuahidi kuwa wananchi wa wilaya yake watautunza vyema hadi utakapokabidhiwa kwa Halmashauri ya Busokelo tarehe 10 Oktoba 2025.
Itunda pia ametumia nafasi hiyo kumpongeza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, na timu yake kwa kazi kubwa na ufanisi waliouonesha katika safari nzima.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzindua miradi mitano yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.3.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako