May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana 1000 kunufaika na ufadhili wa NBC katika masomo ya ufundi

Na Joyce Kasiki,Dodoma

BENKI ya NBC imeanzisha mpango wa ufadhili wa masomo ya ufundi stadi wa’ Wajibika Scholarship’ kupitia vyuo vya Mamlaka ya Ufundi Stadi Nchini (VETA) kwa wanafunzi 1000 ambapo kwa kuanzia benki hiyo  imetenga kiasi cha shilingi milioni 100.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Theobald Sabi mbele ya Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda katika hafla ya kutiliana saini mkataba wa ufadhili huo baina ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia na Benki ya NBC.

 Mkurugenzi huyo amesema,fani zilizolengwa katika ufadhili huo ni pamoja na ushonaji ,uselemara,ufundi wa magari ,ujenzi ,upambaji na fani nyingine huku akisema lengo kubwa ni kuiunga mkono Serikali katika kupanua soko la ajira kwa vijana hapa nchini.

“Changamoto ya ajira kwa vijana ni kilio dunia nzima,na hapa nchini kwetu vijana hutumia muda mwigi kusaka  ajira za kuajiriwa ambazo zimekuwa chache sana,kwa hiyo NBC tukaona tuje na mpango huu ambao baada ya vjana kumaliza masomo yao wataweza kujiajiri wenyewe.”amesema Sabi na kuongeza kuwa

“Leo tunafungua pazia jipya la ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ufundi ili kuongeza nguvukazi ya kuongeza ajira hapa nchini .”alisisitiza

Akizungumza katika hafla hiyo,Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameipongeza Benki ya NBC kwa kuja na mpango huo katika sekta ya elimu huku akishauri mpango huo ulenge katika fani moja ili kwa pamoja waweze kupima matokeo mara baada ya walengwa kuhitimu.

“Naona twende na wazo hili  kwamba kuliko kwenda na fani nyingi,tungechagua fani moja ili tuweze kupima matokeo,na sisi kama Wizara tutaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali washiriki katia jambo hili na kila tutakavyokuwa tunapata wadau tunabadili fani ..,ina maana kama ninyi NBC mkianza na ushonaji basi akipatikana mdau mwingine tutachukua fani nyingine.”amesema Profesa Mkenda

Hata hivyo amesema Wizara haitaiangusha benki hiyo katika utekelezaji wa mpango huo huku akisema wanafunzi watachaguliwa kwa vigezo vinavyotakiwa na siyo vinginevyo.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Anthony Kasore amesema wamepokea mradi huo na fedha ili kutekeleza utoaji ujuzi ambao vijana wengi wa kitanzania wanauhitaji ili waweze kujiajiri na hivyo kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuchangia katika pato la Taifa.