Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imesema tayari imewatambua wabunifu 200 ambao bunifu zao zilifanya vizuri katika Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) katika miaka iliyopita ambapo jumla sh.bilioni 2.3 zimetumika kwa ajili ya kusapoti bunifu hizo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Eliamani Sedoyeka wakati akifungua warsha kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma iliyolenga kuwajengea uwezo kuhusiana na masuala ya ubunifu ili waweze kuelimisha umma kuhusiana na Maonyesho ya MAKISATU ya mwaka huu yanayoatarajia kuanza Mei 15-Mei 20 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Aidha amesema,katika mwaka wa fedha unaoisha Juni mwaka huu serikali ilitenga sh.Bilioni moja katika eneo la ubunifu huku kwa mwaka ujao wa fedha eneo hilo likitengewa kiasi cha sh. bilioni 5.5 .
Profesa Sedoyeka amesema kiasi hicho cha fedha kinatengwa kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ya kubuni na kuendeleza bunifu na kuzijengea uwezo taasisi au mbunifu mmoja mmoja ili bunifu zao ziweze kuingia sokoni.
“Katika mwaka wa 2022/23 Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 5.5 katika masuala ya ubunifu kwa lengo la kuhakikisha wanaboresha mashindano hayo pamoja na bunifu zinazotengenezwa na watanzania.”amesema
Amesema zawadi za washindi katika mashindao ya MAKISATU mwaka huu ni shilingi milioni tano kwa mshindi wa kwanza ,mshindi wa pili shilingi milioni tatu,huku mshindi wa tatu akipata kiasi cha shilingi milioni mbili.
Aidha alisema,wale watakaoingia fainali ya mashindano hayo watapata fursa ya bunifu zao kuendelezwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sayansi,Teknolojia na Ubunfu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Maulilio Kipanyula amesema jumla ya wabunifu 862 wanatarajiwa kushiriki katika maonyesho hayo kutoka katika makundi saba.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanahabari waliopata mafunzo hayo ambaye pia ni Balozi wa Mazingira Sakina AbdulMasoud alisema,watayatumia mafunzo hayo kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya ubunifu.
Aidha amewaasa wanahabari kukumbuka kuelimisha wabunifu kuhusiana na masuala ya utunzaji wa mazingira pindi wanapotengeneza bunifu zao.
Maonyesho ya MAKISATU mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo’ubunifu kwa Maendeleo enedelevu.’
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote