December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viashiria upotevu wa kodi sababu ya ukaguzi wa kodi

Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande ameeleza kuwa ukaguzi au uchunguzi wa masuala ya kodi hufanyika kwa kuzingatia viashiria vya upotevu wa mapato ya Serikali ili kukomboa kodi ambayo haijakusanywa.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kinondoni Mhe. Tarimba Gulam Abbas, aliyetaka kujua ni kwa nini Serikali isiweke ulazima ikiwepo hitaji la Kisheria kuwa uchunguzi wa kodi kwa mlipakodi (Taxpayer Tax Audit) ifanyike kila Mwaka badala ya kusubiri miaka mitatu au zaidi.

Mhe. Chande alisema kuwa Sheria ya Usimamizi wa Kodi, imeainisha mamlaka ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya ukaguzi wa masuala ya kodi kwa walipakodi wote inapoonekana inafaa kufanya hivyo.

“Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwaukaguzi au uchunguzi wa mlipakodi unaweza kufanywa wakati wowote inapoonekana kuna viashiria vya upotevu wa mapato ya Serikali”, alisema Mhe. Chande

Alisema kuwa miongoni mwa viashiria ambavyo hutoa msukumo kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya ukaguzi au uchunguzi wa kodi ni pamoja na mwenendo usioridhisha wa ulipaji kodi.

Alisema viashiria vingine ni pamoja na mlipakodi kutokufuata Sheria za kodi, aina ya biashara au shughuli ya kiuchumi anayofanya mlipakodi husika na suala lingine lolote ambalo Kamishna Mkuu ataona ni muhimu ili kuhakikisha kuwa kodi stahiki inakusanywa.

Aidha Mhe. Chande alisisitiza kuwa ili kupunguza ulazima wa Kamishna Mkuu kufanya uchunguzi au ukaguzi wa mara kwa mara kwa walipakodi, ni muhimu walipakodi wote kuzingatia matakwa ya Sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya kodi iliyopo.

Akieleza kuhusu Serikali kuweka Sheria ambayo itawezesha kufanya uchunguzi wa kodi kwa mlipakodi kila mwaka ili kuondoa wafanyabiashara kubambikiwa kodi kubwa kunakotokana na uchunguzi kutofanywa muda mrefu, Mhe. Chande alisema kuwa Serikali imechukua hoja hiyo na itaifanyia kazi.

Alisema kuwa Serikali itafanya utafiti kuhusu suala hilo bila kuathiri kesi zilizopo Mahakamani zinazohusiana na wafanyabiashara kubambikiwa kodi kubwa kunakotokana na kuchelewa kwa ukakuzi wa kodi.

Alieleza kuwa iwapo Serikali itaona inafaa kufanyia marekebisho sheria iliyopo ya kodi, mapendekezo yatawasilishwa Bungeni na iwapo Bunge litaridhia Sheria itabadilika.