Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online
WASANII wa muziki wa kizazi kipya visiwani Zanzibar wamepatiwa mafunzo maalum ya namna ya kukuza vipaji vyao, pamoja na kutumia sanaa zao kujinufaisha kibiashara.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kisiwani Unguja yalifunguliwa na Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita na kuendeshwa na jopo la wataalamu mbalimbali wa sanaa ya muziki kupitia tamasha la ‘Zuchu Home Coming’ linalotarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Waziri Tabia amewataka wasanii hao kudumisha upendo na ushirikiano pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kuahidi kuzishughulikia changamoto zinazowakabili.
“Hakuna kitu kizuri kama kuwa na taaluma katika kitu kile unachokifanya, ninawapongeza Zuchu na uongozi wa WCB kwa kuona wasanii wa Zanzibar na wao wanafaidika na sanaa ambayo wao wanaifanya,” amesema.
Amesema ni shauku yake kuona anatoa mchango mkubwa katika sanaa, “Tulianza mbali, nataka mtambue kwamba haki na shauku niliyonayo siku nikiondoka wasanii mnikumbuke japo dakika mbili nilizitumia kuwalinda, kuwaheshimisha na kuhakikisha mnapata neema juu ya kazi ambayo mnaifanya.”
Kwa upande wake msanii Zuhura Soud alimaarufu kwa jina la Zuchu amewataka wasanii hao kutumia mitandao ya kijamii kutengeneza fedha kupitia sanaa.
Akitolea mfano amesema kwa mara ya kwanza anapigiwa simu kwamba amewekewa kiasi cha fedha ‘Euro 4000’ hakudhani kama ipo siku angetengeneza fedha mitandaoni.
“Kipindi natoa Zuchu Ep nikapigiwa simu hela yangu ya youtube imeingia, kipindi hicho nilikuwa sijui sana mambo ya Euro inachenjiwa vipi, niliambiwa nimewekewa euro 4000 kwenye akaunti yangu kupitia akaunti ya youtube nikasema aaah hizo zitakuwa ni hela ndogo tu…
“Hapo nimetoka kupewa hela ya nauli Sh20000 na bosi sijaanza kukamata hela, siku moja nikasema ngoja nipite benki, nikauliza euro 4000 ni shilingi ngapi nikaambiwa ni kama milioni 10 nilishangaa sana. Nikaanza kupiga simu mara mbili mbili hiyo ni pesa yangu ya mwezi mmoja siamini, hivyo msishangae ukiona mtu anashangilia kupata viewers milioni 1 youtube ujue anashangilia pesa,” amesema Zuchu.
Naye Meneja wa WCB, Salam Sharafu amesema wasanii wanatakiwa kujituma na kutokukata tamaa, kujiamini mwenyewe ndiyo chapa ‘brand’ anayotakiwa kuitengeneza msanii.
“Kuna msanii hapa Zanzibar ananitumia kila siku kazi zake naziangalia sana na siku zote ninapoziangalia nasema nikija nitamwambia mkubwa Fela, usisubiri mtu akujibu we tuma tu kama mtu anaona kero atakublock lakini ukiona hajakublock endelea kujituma,” amesema Salam.
Naye Miongoni mwa mameneja wa WCB , Said Fella alimaarufu kwa jina la Mkubwa Fella amesema wasanii wanapaswa kujitambua na kujiheshimu huku wakiwa wakweli na kutofake maisha.
“Heshima siyo shkamoo, kama wewe unahitaji kuingia katika muziki basi fahamu kwamba kuna watu nimewakuta wanahitaji kufahamu mimi ni nani lakini nisipitilize. Lakini kuna muda sanaa itakulazimisha wewe uwapite, jambo la pili itakubidi uwe mkweli wa maisha yako, wengi wanafeki na wengine kufake mpaka kupitiliza lazima uanguke tu.”
More Stories
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi
Rais Samia apongezwa kwa miongozo madhubuti ya ukusanyaji wa kodi
Mwenda:Siku ya shukrani kwa mlipakodi ni maalum kwaajili ya kuwatambua,kuwashukuru