Na Mwandishi Wetu, Kilwa
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema sasa ni wakati mwafaka kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne, Benard Membe kujiunga na upinzani nchini.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kilwa, Zitto amesema mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mbunge na waziri wa wizara nyeti hapa nchini ana fursa ya kuunganisha Watanzania wenye kiu ya mabadiliko kupitia vyama mbadala vya siasa.
“Ndugu yangu Benard Membe kafukuzwa uanachama wa CCM. Ninajua bado anatetea haki yake ya uanachama huko. Ni hatua sahihi.
Hata hivyo muda wa kuleta mabadiliko katika nchi umewadia, ninamsihi afanye maamuzi ya kuunganisha nguvu kupitia vyama mbadala ili kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka,” amesema.
Kiongozi huyo wa ACT ambaye yuko katika ziara ya kichama ya mikutano ya ndani Kusini mwa Tanzania, amesema anaelewa mwanasiasa huyo bado anapambana kubaki ndani ya CCM, lakini muda huu anahitajika zaidi kwenye upinzani.
Membe, mmoja wa wanasiasa mashuhuri nchini, alifukuzwa uanachama wake CCM miezi michache iliyopita na hali yake kwa sasa iko kwenye sintofahamu.
Akizungumza na redio Sauti ya Ujerumani (DW) hivi karibuni, Membe alisema ingawa kwa sasa bado anaangalia hatma yake ndani ya CCM, upo uwezekano wa kuwania urais kupitia vyama vingine mbadala.
Zitto amesema historia itamhukumu vibaya mwanasiasa huyo endapo hatafanya uamuzi wa kujiunga na upinzani sasa. “Mimi najua Membe anaipenda Tanzania na ni Mwana demokrasia. Adhihirishe mapenzi yake kwa nchi yetu kwa kuongeza nguvu wa vyama mbadala.
“Kama kuna kosa la uhaini basi itakuwa ni kwa Membe kutofanya maamuzi ya kuwatumikia Watanzania nje ya CCM. Ninamsihi kuwa afanye tafakari na kufanya maamuzi sahihi na wananchi,” amesema Zitto huku akishangiliwa na umati uliohudhuria mkutano huo.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito