January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zinedine Zidane aipa kisogo Real Madrid

MADRID, Uhispania

KLABU ya Real Madrid, imetangaza kuwa kocha wake mkuu Zinedine Zidane, ameamua kuondoka katika klabu hiyo baada ya kumaliza kipindi chake cha pili kama meneja huku akitoka bula ya kunyakuwa ubingwa.

Kuondoka kwa Zidane kunafuatia msimu wa kukatisha tamaa kwa klabu hiyo, ambao walishindwa na wapinzani wao Atletico Madrid katika mbio za kuwania taji la Ligi Kuu Uhispania La Liga, iliyokwenda hadi siku ya mwisho.

Mbali na hivyo, pia Real Madrid waliondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na Chelsea katika nusu fainali kwani walishindwa kushinda kombe kwa mara ya kwanza katika misimu 11.

Zidane alirejea Real Madrid mnamo Machi 2019, akichukua nafasi ya Santiago Solari, na akashinda taji lake la pili la La Liga katika msimu ulioathiriwa na Covid wa 2019-20. Katika kipindi chake cha kwanza klabuni hapo Januari 2016 hadi Mei 2018, Zidane alishinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa na ligi ya Uhispania 2016-17.

Mfaransa huyo amewaambia wachezaji wake na wasaidizi wake kuwa anaondoka, na alimjulisha Rais wa klabu hiyo, Florentino Pérez juu ya uamuzi wake.

%%%%%%%%%%%%%