Na Jakline Martin, TimesMajira Online
OKTOBA 22, Mwaka huu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilimteua Paul Makonda kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi akichukua nafasi ya Sophia Mjema.
Baada ya uteuzi wake, Makonda alifanya ziara ya kwanza ya kujitambulisha ilioanza Novemba 9, 2023 na ilihitimika Novemba 15, 2023 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Mara.
Kupiti ziara hiyo, Makonda aliacha ujumbe mzito kwa watendaji wa Serikali hususani kuwatumikia wananchi kwa moyo na bila kuwabagua.
Katika awamu hii ya pili ya ziara yake Makonda amefanya katika mikoa 10, ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga na Simiyu kuanzia Desemba 19 hadi 31, Mwaka huu.
Katika ziara anazozifanya amekuwa akisikiliza kero za wananchi na kuzitatua, kwa kutoa maagizo ya Chama kwa viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wakurugenzi, Wakuu a Mikoa na Wilaya na watendaji wengine wa Serikali na chama.
Stahili yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi imeacha somo kubwa kwa watumishi wa Chama na Serikali hususani kwenye suala la kutenga muda wa kusikiliza kero za wananchi.
Januari 19, 2024 Makonda akiwa mkoani Dar es Salaam alimpigia simu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na kumpa maagizo ya chama kufika Bunju ili kutatua migogoro inayowakabili wakazi wa eneo hilo baada ya kupokea malalamiko juu ya suala hiyo.
Katika kutekeleza hilo,Waziri Silaa Januari 19, 2024 alifika maeneo hayo na kuwataka wasajili wa Hati wa Ofisi za Kamishna wa Ardhi Dar es salaam na Pwani kuacha urasimu kabla hajaanza kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Waziri Silaa aliwapa siku mbili za kubadilika kwa kutoa miamala ya hati haraka na kwa wakati bila urasimu.
Anasema watumishi hao wamekithiri kwa lugha chafu na zisizo ridhisha kwa wananchi wanaotaka huduma katika ofisi hiyo, ambayo ndio inahusika na kuandaa na kutoa hatimiliki za ardhi pamoja na miamala mingine ya kisheria kwa wananchi.
Aidha, anasema hatamuamisha mtu kwa uzembe na badala yake atawachukulia hatua kali za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi watakao bainika na maelekezo hayo ameishampa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
Wakati Makonda akiwa mkoa wa Tanga, Januari 20, Mwaka huu alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusu kuzuiwa maiti za ndugu zao kwa kushindwa kulipa deni.
Kutokana na changamoto hiyo, Makonda alimtaka Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutoa kauli ya Serikali kuhusiana na kero hiyo.
Waziri Ummy anasema, “Marufuku kuzuia maiti ya Mtanzania yeyote ,Kwa hiyo nawataka waganga wafawidhi wa hospitali zote nchini kwa kufuata miongozo ya Serikali ni marufuku kuzuia maiti, naomba nirudie katika mkutano wako kulisisitiza hili,”anasema Ummy.
Aidha Makonda anatoa wito wananchi wote ambao kero zao hazikutatuliwa wafike ofisi za halmashauri ya jiji mapema asubuhi ili kwa pamoja asikilize kero zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Rajabu Abdulrahman anasema anamshukuru Mwenezi kwa niaba ya wananchi wote wao pia kama viongozi wamejipanga kuungana naye kutatua kero mbalimbali
“Nikushukuru kwa niaba ya wananchi wote wa mkoa wa Tanga ,kwenye kuwapunguzia au kutatua kero mbalimbali, kama viongozi wajibu wetu ni kuangalia namna nzuri ya kutatua migogoro hiyo,” anasema Abdulrahman.
Katika hatua nyingine CCM iliamuru Katibu na Mwenyekiti wa wilaya kurudisha nyumba ya Mzee aliyefahamika kwa jina la Nassor Fahed anayedai kunyang’anywa nyumba yake iliyopo Tanga Mjini na Chama hicho.
“Katibu wa wilaya, mwenyekiti wa wilaya una dakika mbili nyumba irudi kwake leo,”anasema Makonda
Sambamba na hayo, Makonda alibidhi sh.500,000 kwa Bibi aliyefamika kwa jina la Herena Bakari aliyewasilisha kero yake kuhusu changamoto ya afya pamoja na makazi duni.
“Ummy (Waziri wa Afya) alikuja kwangu, mguu huu nimekanyagwa na pikipiki siwezi kulala ,mimi nalia mnisaidie Serikali siwezi kutembea nina miaka 100 , Nisaidie mimi leo hapa nina usingizi nikalale, Ummy wangu sijui yuko wapi ,” anasema Herena.
Makonda alipendekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Pangani mkoani Tanga, Isaya Mbenje asimamishwe kazi baada ya kuwa na tuhuma nyingi kutoka kwa wananchi mbalimbali.
“Nimetoka Pangani nilikuta kero nyingi zinasababishwa na Mkurugenzi wakati nakuja njiani nimempigia simu Waziri wa TAMISEMI nikamwambia mapendekezo ya Chama Cha Mapinduzi Mkurugenzi wa Pangani asimamishwe kazi,” anasema.
Muda mfupi baada ya Chama hicho kutoa pendekezo hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga,Isaya Mbenje ili kupisha uchunguzi.
Aidha, Makonda alipatia sh. Milioni moja mkazi wa eneo la Kwasemangube lilipo Korogwe Mjini ,Mkoani Tanga aliyefahamika kwa jina la Yohana Kihiyo aliyekatwa mguu wake kutokana na changamoto ya ugonjwa wa kisukari.
“Hii hela natoa kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama Dkt. Samia kuna watu wanapambana kuzuia watu fulani wasipate kazi wengine wanakwenda mpaka kwa waganga wa kienyeji ,jamani hamzuii tu hao watu mpaka baraka za watu wenye uhitaji ,halafu nitakutafutia kiti kizuri kinachotumia umeme chenye thamani ya milioni Tano,” alisema.
Yohana aliwasilisha kero zake kwa Makonda ,kwa kueleza changamoto anazozipitia ikiwemo suala la bima ya afya na mahali pa Kuishi baada ya mke wake kufariki.
Wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Jimbo la Same Magharibi, wananchi wa jimbo hilo walimkataa Mbunge wa jimbo hilo, Mathayo David Mathayo mbele ya Makonda kwa madai ya kuwa hawasaidii wananchi katika baadhi ya shughuli kwa ajili ya maendeleo ya jimbo hilo.
Raphael Mrutu, ambaye ni mkulima na mkazi wa Same anasema kama chama hakitawasikiliza madai yao, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu yatakuwa ya kushangaza sana.
“Mwenezi hatumtaki mbunge wetu wa hapa (Mathayo), hapa tuna mkuu wa wilaya na mkurugenzi hatuna mbunge, kwa sababu amewagawa wananchi kwa baadhi ya matendo yake hatumtakii tusaidie hapa tuna Mbunge ambaye Bungeni hatumuoni na kwenye Jimbo hatumuoni,” anasema Mrutu.
Akijibu kilio hicho, Makonda aalisema kipimo cha mwisho kuwa kipimo cha CCM kumpitisha kiongozi ni kumpima namna anavyowasaidia wananchi wake na kuleta maendeleo katika maeneo wanayoyaongoza na si vinginevyo.
Alisema Chama hicho kimejipanga kuwashughulikia viongozi wote wasiofanya shughuli za kimaendeleo kwa wananchi na badala yake wamekaa wakisubiria kutoa posho na kanga kwa wajumbe ili wapate ridhaa ya kuongoza.
Katika jimbo la Moshi Mjini, Makonda anaeleza kukerwa na ujenzi wa Kituo Kikuu cha Kisasa cha mabasi kutokamilika kwa wakati kutokana na uzembe wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
“Mradi huu ulikwama kutokana na makosa yaliyofanywa na uongozi wa Manispaa ya Moshi Mjini kwa kutomlipa mkandarasi kwa wakati na ilisababisha hasara kwa Manispaa hiyo baada ya kutakiwa kulipa fidia kwa mkandarasi baada ya kucheleweshewa malipo yake kulingana na mkataba uliokuwepo,” anaeleza Makonda.
Makonda akiwa Tabora alibaini chanzo cha kero, changamoto na migogoro ya ardhi ni uzembe wa wakurugenzi na watumishi wa Serikalini na kubainisha kuwa tatizo kubwa linalopelekea wananchi kutokuwa na upendo na Serikali yao inayotokana na Chama Cha Mapinduzi ni uzembe wa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri na Watumishi wa Taasisi mbalimbali za Kiserikali.
Makonda anasema, Chama Cha Mapinduzi hakitafumbia macho Mtumishi yeyote wa Serikali anayekuwa chanzo cha migogoro au kero zinazopelekea wananchi kuichukia Serikali na kupelekea kukichukia Chama Cha Mapinduzi na hatimaye kupunguza imani yao kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Anasema hiyo ndio maana halisi ya Chama Cha Mapinduzi kuwa kazini.
Aidha, Mwenezi Makonda anaeleza umma ya kwamba Rais Dkt. Samia ana dhamira za dhati katika kuongoza nchi na anaongoza akiwa na hofu ya Mungu na ndio maana anaongoza kwa kanuni yake ya 4R.
Pia amekuwa akitoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo lakini baadhi ya watumishi na watendaji wamekuwa wakifanya uzembe na wengine kwa makusudi.
Hivyo aliwaomba kuendelea kumuamini Rais Samia na Chama Cha Mapinduzi, kwani kwa kutambu hilo ndio maana amekituma chama kupitia yeye (mwenezi makonda) ili kuipelekea Serikali maabara kupata kujua shida ilipo na kuitibu.
***Zaimuibua Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt Eliezer Feleshi, ameshtushwa na wingi wa watu wenye malalamika ya kudhulumiwa haki na utekaji wa ndugu zao kwenye ziara za Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda.
Jaji Feleshi alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika jijini Dodoma.
“Mimi napenda utafiti, kati ya vitu nilivyoshangaa mambo niliyoyasikia labda miaka 15 nyuma bado hayo hayo wananchi wanayalalamikia, nikifuatilia ziara ya yule katibu wa itikadi wa Chama cha Mapinduzi (Makonda) naona wananchi bado wanajisomba kwake kama mafuriko.
“Hivyo hivyo ukifuatilia nyumba za ibada wananchi wanajisomba huko, kwa hiyo hii sasa mheshimiwa Rais tunaichukulia kama changamoto, pamoja na kusoma kwetu, pamoja na kupata nyenzo na maboresho tunayoendelea nayo, tujue wananchi wanahitaji kupata kile wanachokusudia kukipata.” Alisema Jaji Feleshi.
Alizidi kusema kwamba; “Kwa minajili hii mheshimiwa Rais wewe ndiye mlezi wa ofisi yetu na taasisi za kiserikali, tumekusudia vile vile tuwe na vituo vya huduma wezeshi saa 24.
Yeyote aliyekosa huduma mahala afike kwenye hicho kituo na kuelekezwa taratibu za kuchukua. Na sisi tutanzia hapa Dodoma nafikiri tutaomba usaidizi wa kibajeti, ikiwezekana mwaka huu unaokuja wa fedha.
Kituo hicho cha kwanza jumuishi kianze, mtu ambaye kafungiwa mlango sehemu fulani, basi apewe yale maelezo yote ya msingi, ilimradi tupunguze huu utitiri wa watu kwenda mahala pasipostahili.”
Tangu aanze ziara zake kwenye mikoa 20 iliyopewa jina la Back 2 Back, Makonda amekuwa akisikiliza kero ambalimbali za wananchi ikiwemo kudhulumiwa haki zao na utekaji.
Miongoni mwao wanalalamikia vyombo vya kutenda haki, kutotenda haki au kivituhumu katika baadhi ya maeneo.
Mfano katika baadhi ya mikoa alipokea malalamiko ya watu kupotea tangu mwaka 2021 na wengine walitoweka kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana tangu mwaka 2022 na mwaka jana.
Wananchi hao wamedai malalamiko yao yanafahamika kwenye vituo vya polisi na hata serikalini, kwani hata makamanda wa Polisi walipoulizwa walikiri kuyafahamu na kutaja hata namba za majalada ya kesi zao.
Wengine wamekuwa wakidai kwamba wanapokwenda polisi kuulizia upelelezi wa kufuatilia ndugu zao au waume zao umefikia wapi? Wao ndiyo wanaoulizwa wana taarifa gani mpya wakati wao hawana mamlaka ya kufanya uchunguzi.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia