November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara za CCM ni taswira nzuri ya Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WAKATI ziara za Katibu wa Itikadi na Uenezi, Paul Makonda ikiendelea katika Mikao mbalimbali imedhihirisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kina kila sababu ya kujidai,kujisikia vizuri,kuringa na kila aina ya deko kwa sababu ya wingi wa watu wanaohudhuria ama kwa lugha ya kisiasa iliyozoeleka wakati wa uchaguzi ya “nyomi”.

Katika ziara hizi tumepata mambo kadhaa ambayo yanapaswa kujadiliwa katika uga wa kisiasa.

Matumaini; maelfu ya wananchi wanaohudhuria mikutano ya hadhara inayofanyika na kumsikiliza Paul Makonda wanaonesha kuwa wanayo matumaini kwa Chama cha Mapinduzi.

Wengi wa wananchi wanaoeleza mambo yao au kero yoyote inayosikilizwa na Katibu huyo inaonesha dhahiri kuwa matumaini ya wananchi hao ni makubwa kwa CCM.

Jambo hili pekee lina manufaa kwa CCM chenyewe kuona namna bora ya kuendelea kuwafurahisha na kusikiliza kero na kutatua kama wafanyavyo kila mara.

Matumaini ni sehemu ya binadamu na kawaida watu hao huwa na ustahimilivu. Kuanzia mwanzo wa mkutano hadi mwisho, utaona kuwa CCM inasikilizwa na Katibu wake anasikilizwa.

Mkono wa kulia wa Mwenyekiti Rais Samia; kwa mujibu wa taratibu za CCM Rais anayekuwepo madarakani ndiye anapaswa kuwa Mwenyekiti wa Chama, hivyo Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kiongozi mkuu wa chama hicho anaonekana kwenye mikutano ya hadhara inayofanywa na Paul Makonda Kwamba Katibu huyo ndiye mkono wa kulia wa Mwenyekiti wa CCM.

Ndiye anawakilisha sera na maono ya chama kwa wananchi.


Anachosikiliza ni sawa na sikio la Rais Samia lipo kwenye mikutano hiyo ya hadhara na kuwafanya wananchi kuona umuhimu wa kupata fursa ya kuwasilisha lalamiko aua chochote kile kwa Katibu huyo wakiwa na imani ndiye anamwakilisha Rais Samia kupitia CCM.

Katika hatua hiyo jicho la Rais Samia linakuwa linazunguka Mkoa kwa Mkoa, Wilaya kwa Wilaya kwa ajili ya kuelewa na kuzungumza na wapigakura wao.

Hadi hapo utaona kuwa ziara hizi zinamwakilisha vema Rais Samia kisiasa na kuongeza nguvu ya CCM katika maeneo mbalimbali nchini.

Watanzania wanapenda siasa; katika hali ambayo unaweza kuhitimisha wananchi wanapenda siasa na wanawapenda viongozi wao wanaoongoza nchi.

Kila nikitazama aina ya watu wanaohudhuria mikutano hiyo si ya wale wanachama wa CCM peke yao, bali hata wale ambao ni wakazi wa maeneo ambayo mikutano inafanyika.

Watanzania wanapenda siasa kwa maana ya hatua ya kuhudhuria na kusikiliza hotuba za mikutano ya kisiasa namna ile kuanzia Mwanza, Shinyanga, Ruvuma, Iringa na maeneo mengine ni dhahiri watu wanapenda na kusikiliza nini viongozi wao wanauzngumza na kuwapa imani kuwa wapo pamoja nao.

Paul Makonda kama Katapila; Katibu huyu amekuwa akipeperusha bendera ya chama chake, katika namna ambayo unaweza kusema kazi ngumu mpe Paul Makonda.

Pengine ingemuwia vigumu kujenga ushawishi, lakini Paul Makonda bila kujali hoja zake anatumia lugha ambayo inawavuta watu kusikiliza na kuelewa anachowalisha.

Pengine wanazuoni wangeweza kusema kuwa hotuba za Paul Makonda si kutatua kero bali siasa.

Lakini wanasahau kuwa ni siasa ndiyo inayofanya kazi ya kuleta huduma na maendeleo kwa nchi yoyote (kama nilivyoeleza hapo awali kuwa ni mkono wa kulia wa Mwenyekiti wa Chama).

Kila chama kinafanya shughuli za kisiasa, ndiyo maana wakati wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, tulishuhudia Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana akizunguka sehemu mbalimbali mikoani kukagua shughuli za maendeleo pamoja na uhai wa chama.

Ziara zile zinafanana kabisa na hiki kinachofanywa na Paul Makonda zikiwa na ninia ileile ya kuendeleza na kuimarisha chama pamoja na kuwaweka karibu wanachama na wananchi wao. Katika nukta hiyo shughuli ya kuwavutia wapigakura katika kipindi hiki ni ishara kuwa mahudhurio hayo ni kipimo kingine cha mvuto wa CCM miongoni mwa wananchi.

Ni dhahiri bila hata kuandika ripoti ya ziara yake kwenda kwa Mwenyekiti wa CCM, inaonekana kabisa viongozi wa juu wanaona kila hatua inayoonekana katika vyombo vya habari kuanzia Televisheni, magazeti na vyombo vya habari vya mitandaoni.

Thamani ya viongozi wa chini. Unapoona kiongozi wa juu kabisa akiwafuata wenzake walioko chini mfano mikoani na wilayani, ni hatua muhimu katika kujenga chama.

Kwamba viongozi wa mikoani na wilayani wapo kairbu na wananchi na wanatambua njia nzuri ya kutafuta kero na kumsaidia Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika nukta hii inaonesha kuwa wananchi wanamsikiliza Katibu huyu kama nembo ya chama kinachounda serikali ya awamu ya sita.

Kwamba viongozi wa ngazi za chini wanashiriki kupitia chama kumsaidia Rais Samia kwa kujibu hoja za wananchi pamoja na kuchunguza kwa undani kama mirdai ya maendeleo inatekelezwa kama ilivyoagizwa.

Nafuu wanayopata viongozi wa ngazi za chini ni ile hali ya kusaidiwa kumaliza kero kadhaa ambazo zimekuwa sugu au zinahitaji uongozi wa juu wa chama kuzitambua na kuishauri serikali juu ya njia bora ya kutatua.

Ajenda ya kuandika ilani; katika ziara Paul Makonda kila hotuba na mazungumzo yake na wananchi ni sehemu nyingine ambayo CCM wanaweza kutumia kuandaa ilani ya uchaguzi wa mwaka 2025.

Ilani ya uchaguzi inakuwa ya miaka mitano, na mikutano hii inatengeneza ajenda ya kuandika ilani ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Kwa kawaida lazima ilani iandikwe kwa kupitia mikutano ya hadhara ambako Katibu anasikiliza wananchi na wanachama, huku jopo la watafiti wa CCM wanaweza kutumia kama nyenzo ya kuelewa saikolojia waliyonayo wapigakura.

Vilevile ni sehemu muhimu ya kuvumbua mahitaji ya mapya ya wananchi pamoja na kubashiri nini kipya kinaweza kufanyika na kuingizwa katika ilani ijayo.

Kwa hatua hii ni kongole nyingi kwa CCM na uongozi wake kuhakikisha wanawafuata wananchi kila mahali na kuzungumza nao.

Mazungunmzo hayo ndiyo yanatengeneza matumaini, imani na kuwasilisha ajenda za msingi za kisiasa,uchumi na maendeleo kwa maslahi ya Tanzania.

CCM wanapuliza manukato mazuri kwa wananchi na mwitiko unaonekana jinsi walivyo na imani na matumaini.