Na Mwandishi Wetu, TimesMajiraOnline, Dar
WIKI iliyopita Novemba 16, mwaka huu Rais wa Romania, Klaus Iohannis, aliwasili nchini kwa ziara ya Kitaifa ambayo ilimalizika Novemba 19, 2023 kufuatia mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ziara hiyo ya Rais Iohannis ni mfululizo wa ziara za wakuu wa nchi mbalimbali nchini ambazo ni matokeo ya uongozi thabiti wa Rais Samia.
Ziara hizo za viongozi hao zimefungua fursa nyingi za kiuchumi na nyingine nyingi.
Ziara ya Rais Iohannis imekuwa ni ya kihistoria na ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa Taifa hilo kutembelea nchini, kwani imesaidia kuimarisha ushirikiano katika maeneno ya kimkakati ikiwa ni pamoja na kushawishi uwekezaji zaidi na kuvutia watalii wengi kutoka nchini Romania.
Ndiyo maana Rais Iohannis na mwenyeji wake, Rais Samia katika mazungumzo yao yaliyofanyika Novemba 17, mwaka watajadili namna bora ya kukuza na kuimarisha ushirikiano kati sekta za elimu, afya, kilimo nishati na madini.
RAIS Samia mwenyewe anakiroi kwa kutaja ziara ya Rais Iohannis kuwa ni ya kihistoria na ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa Taifa hilo kutembelea nchini na imesaidia kuimarisha ushirikiano katika maeneno ya kimkakati.
Rais Samia anasema katika mazungumzo na mgeni wake wamekubaliana kuwa mataifa yao yataimarisha ushirikiano katika sekta za afya, hususan utengenezaji wa dawa, usindikaji wa mazao ya kilimo, madini pamoja na mbinu za kukabiliana na majanga.
Maeneo mengine ya ushirikiano ambayo viongozi hao wamedhamiria kuyapa kipaumbele ni ufadhili wa masomo, ambapo Romania itatoa nafasi 10 kwa ajili ya Watanzania kusoma masomo ya udaktari na ufamasia katika mwaka huu wa masomo.
Aidha, Tanzania imetoa nafasi tano za masomo kwa wanafunzi wa Romania kuja kusoma nchini katika vyuo watakavyochagua wenyewe.
Rais Samia anaongeza kuwa nchi hizo zimedhamiria kukuza kiwango cha biashara na uwekezaji ambacho kwa sasa hakiridhishi licha ya nchi zao kuwa na fursa nyingi za uwekezaji.
Viongozi hao wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya kimataifa na hasa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo itajadiliwa kwa kina katika mkutano wa COP28 uliopangwa kufanyika Umoja wa Falme za Kiarabu mwishoni mwa mwezi Novemba 2023.
Naye Rais wa Romania, Iohannis anasema Romania imekuwa na ushirikiano mzuri na imara wakati wote, na lengo la ziara yake nchini Tanzania ni kuimarisha zaidi uhusiano baina ya mataifa hayo.
“Tumekuwa na uhusiano mzuri na imara wakati wote, na katika kuendelea kuimarisha uhusianoi wetu tumekubaliana kuimarisha uhusianio wetu kwenye maeneo ya kimkakati na Tanzania katika sekta za kilimo, ulinzi wa raia, ulinzi wa kimtandao, teknolojia na uchumi,” anasema Rais Iohannis na kuongeza;
“Kusainiwa na hati hizi mbili za makubaliano ya ushirikiano ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wetu.”
Pamoja na mambo mengine, Rais Iohannis anasema kuwa Romania itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mambo waliyokubaliana kwa maslahi ya mapana ya pande zote mbili.
Wakizungumza na gazeti hili, Watanzania wa kada mbalimbali wamempongeza Rais Samia kwa kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali.
Wamesema huu ni wakati muafaka kwa viongozi serikali kutumia fursa hiyo iliyofunguliwa na Rais Samia ambapo viongozi kimataifa wanaokuja nchini kujenga mahusiano mazuri kwa ajili ya kuendeleza diplomasia na ushirikiano wa kimataifa ili taifa letu lizidi kunufaika na ziara hizo.
Mchumi John Samuel, anasema kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Romania, Lohannis,kutembelea Tanzania, ikiwa ni ziara ya kwanza wa kiongozi mkuu wa nchi hiyo kutembelea Tanzania ni kielelezo kuwa Rais Samia ameimarisha ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingi duniana, hivyo Watanzania wanaendelea kukipata kutokana na ziara hizo ni zaidi ya fursa.
“Ziara ya Rais Iohannis ni muendelezo wa viongozi kutoka mataifa mbalimbali kuitembelea Tanzania suala linalo thibitisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na mataifa ya kigeni,” anasema Samuel na kuongeza;
“Ili kupatikana manufaa ya ujio wa rais wa Romania na wakuu wa nchi wengine, ni lazima wasaidizi wa Rais Samia waelewa na kutekeleza kwa vitendo falsafa ya kuongozi huyo, kwani viongozi wa Serikali wanapaswa kujenga mahusiano mazurina mataifa hayo.”
Naye Dkt. Matungwa Katabazi, anasema kuna haja kwa Serikali na viongozi walio karibu na Rais Samia kujenga mahusiano na wale wanaokuja nchini ili nchi yetu iweze kufaidika kielimu na kiuchumi.
Anasema Tanzania na Romania zimekuwa zikishirikiana kwenye masuala mbalimbali ikiwemo biashara ambapo mwaka 2021 Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 7.9 ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo iliuza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 4.06.
Anasema hiyo inaonesha kushuka kwa ushirikiano wa kibiashara kwa kipindi cha hivi karibuni, hivyo ziara ya Rais Iohannis, itaimarisha zaidi ushirikiano.
Balozi Samweli Shelukindo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema ziara hiyo inatarajiwa kuongeza fursa za masoko na biashara baada ya mikataba mbalimbali kusainiwa.
“Tuna matumaini makubwa kwamba ziara hii itafungua fursa kubwa sana za masoko na tunategemea kwamba kusainiwa mikataba michache ya kukuza mahusiano katika sekta ambazo tunafikiria tunaweza kupata faida kubwa,” anasema Shelukindo.
Mkazi wa Kawe, jijini Dar es Salaam, Paul Emmanuel anasema endapo yale yaliyozungumzwa na Marais hao yatatekelezwa, kutakuwa na ongezeko la mnyororo wa thamani wa bidhaa, biashara pamoja na kilimo.
More Stories
Tanzania Yaibuka Kidedea: Uongozi wa Rais Samia waboresha weledi wa Jeshi la Polisi
Tuhimize amani kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024
Ana ahidi,ana tekeleza,maneno kidogo,vitendo vingi