Na Agnes Alcardo
TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazoelezewa vizuri kwa kufuata na kujali demokrasia katika masuala ya siasa, hususani katika kipindi cha Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kama inavyofahamika, mara nyingi siasa zimekuwa moja ya sababu kubwa zinazoligawa taifa, kutokana na uongozi uliopo madarakani kulegalega katika usimamizi mzuri wa kuvipa uhuru vyama vya upinzani katika kutoa maoni, kuikosoa serikali pale inapoonekana kutofanya vizuri. Hata hivyo, Tanzania imesimamia demekrasia kwa asilimia kubwa.
Serikali iliyopo madarakani chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inaendelea kufanya kazi kubwa kupitia viongozi wake kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na maendeleo na zinafanyika siasa safi na za kistaarabu lakini pia katika kuimarisha Chama, viongozi wa CCM ngazi za juu wameteuliwa ili chama hicho kiendelee kuimarika.
Miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu waliopata nafasi hiyo ni Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA. Amos Makalla.
Mbali na kupata uteuzi huo, CPA. Makalla, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Juni 30, 2024 Ofisi ndogo za Chama, Jijini Dar es Salaam kilimteua kuwa Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, ili wanachama waendelee kulelewa na kukomaa katika misingi imara ya kichama chini ya jemedali huyo.
NAFASI ALIZOWAHI KUSHIKA SERIKALINI NA KATIKA CHAMA
CPA. Makalla ni miongoni mwa viongozi waliowahi kushika nafasi mbalimbali za kiuongozi nchini. Kati ya nafasi hizo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya na Katavi na Naibu Waziri wa Habari, huku akiwa Mbunge wa Mvomero katika vipindi tofauti, ambapo kwa mara ya mwisho kuwatumikia wananchi wa Mvomero ilikuwa ni mwaka 2015.
Inaelezwa kuwa, CPA Makalla ni mwanasiasa mkongwe, mwenye maono, misimamo na asiyependa kuyumbishwa katika maamuzi huku akiwa ni zao lililotokana na (CCM) na kati ya nafasi za kiuongozi ambazo amewahi kushika ndani ya chama hicho ni pamoja na kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha, Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), kukaimu nafasi ya Katibu wa Umoja wa Vijana CCM na sasa ni Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa.
SAFARI YA SIASA
Waswahili usema: ‘Mcheza kwao hutunzwa’ na hii inajidhihirisha wazi kwa CPA. Makalla kuwa, kati ya sehemu nzuri za uongozi anazozitendea haki katika uongozi wake basi ni katika upande wa siasa! hususan katika Jiji la Dar es Salaam ndani ya chama kwa maana nyingine kama ni kiatu basi hiki ndiyo saizi yake.
CPA. Makalla tangu kuteuliwa kwake katika nafasi ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, yapo mambo mengi ameyafanya ya kimaendeleo katika Chama hususan kusikiliza na kutatua kero za wananchi Dar es Salaam, baada ya kufanya ziara yake ya kichama katika wilaya za mkoa huo.
KUTEMBELEA NA KUKAGUA MIRADI
Julai 6, mwaka huu, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa na Mlezi wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, CPA. Makalla, alianza ziara yake ya Kichama mkoani humo kwa kuanza kukutana na wana-CCM na viongozi wa Chama na Serikali na kuzindua na kutembelea miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo ililenga kuangalia uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020/2025, kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kuangalia hali ya Chama kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
CPA Makalla akiongozana na viongozi mbalimbali wa ngazi husika wa Chama na serikali, alifanikiwa kuyafikia majimbo sita ya uchaguzi ya Ukonga, Segerea, Ubungo, Kinondoni, Kawe na Kibamba.
Ziara hiyo aliianza katika majimbo yaliyopo Wilaya ya Ilala ambayo ni Ukonga, Segerea na Ilala na kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara za mitaa ya Mwanza na Kigoma, zinazojengwa kwa kiwango cha lami, mifereji na taa za barabarani, ambazo tayari ujenzi wake umefikia asilimia 90 hadi sasa, huku akimtaka mkandarasi kuongeza kasi zikamilike ndani ya muda uliopangwa.
Pia, alitembelea na kukagua jengo jipya la wazazi lililopo Kituo cha Afya cha Kinyerezi, ambapo alifurahishwa na maendeleo hayo.
Makalla alisema, awali kituo hicho kabla ya kupanda hadhi kilitambulika kama zahanati na kuwataka watendaji na watoa huduma kuongeza bidii katika kuwahudumia wagonjwa na kutumia lugha nzuri, wananchi wajivunie maendeleo hayo, huku akisisitiza sifa zote za maendeleo yanayoletwa nchini kuwa ni za Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia.
Aidha, alitembelea mradi wa maji wa Bangulo wenye ujazo wa lita milioni tisa, ukiwa na thamani ya sh. bilioni 36, ukiwa unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu. Kukamilika kwa mradi huo, kutaondoa kero ya upatikanaji wa maji kwa wananchi walio pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam.
Pia, alitembelea stendi mpya ya mabasi yatakayokuwa yakiingia na kutoka Chanika na kusema kutokana na kukamilika kwa stendi hiyo kutawasaidia wakazi wa maeneo hayo kutopata usumbufu wa kwenda mbali kufuata usafiri.
Aidha, alitembelea jengo la ghorofa la Shule ya Sekondari Mnazi mmoja, Shule ya Sekondari Minazi Mirefu na Shule ya Sekondari Liwiti, huku akiwataka wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri kuwaondoa wakandarasi wanaokwamisha kukamilika kwa miradi hiyo.
Akiwa wilayani Kinondoni, CPA Makalla, alitembelea na kukagua Kituo kipya cha mabasi cha Mwenge, ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 99, ambacho kitaongeza ajira, mzunguko wa biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa Kinondoni na Tanzania kwa ujumla.
Sambamba na hilo, pia alitembelea na kukagua Uwanja Mpya wa Mpira wa KMC unaodhaminiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, ambapo aliipongeza Wilaya ya Kinondoni kwa uthubutu mzuri waliofanya katika kutumia fedha za mapato ya ndani kuwekeza sekta mbalimbali ikiwemo ya michezo.
CPA Makalla pia, alitembelea na kuzindua jengo la wodi ya wazazi liliyopo Kituo cha Afya cha Nyakasangwe, huku kituo hicho kikionekana kuwa mkombozi kwa wananchi wa Madale ambao awali hawakuwa na kituo cha afya, hali iliyowalazimu kwenda maeneo ya mbali kupata huduma za afya.
Katika ziara hiyo pia, alitembelea na kukagua jengo jipya lenye wodi ya wazazi katika Hospitali ya Sinza Palestina, huku akielekeza mamlaka husika kuboresha miundombinu ya njia za kupita ndani ya hospitali hiyo kuwarahisishia wagonjwa na wanaofika kupata huduma na kufungua jengo la Ofisi za CCM Tawi la Makumbusho.
Akiwa katika Wilaya ya Ubungo, alitembelea na kukagua mradi wa Kituo Cha Biashara na Usafirishaji, East Africa Commercial and Logistic Center (EACLC), mradi mkubwa wa biashara utakaowasaidia wafanyabiashara nchini na nchi za jitani kupata kila aina ya biashara nchini Tanzania badala ya kwenda kufuata bidhaa China.
Mradi huo ambao unaelezwa kusimama kwa takriban zaidi ya miaka 10, hivi sasa unaendelea kukamilishwa katika hatua za mwisho chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia, huku miongozi mwa waliotoa mapendekezo ya uendelezwaji wa mradi huo akiwa CPA Makalla.
Mwenezi CPA Makalla pia, alitembelea Shule ya Sekondari ya kisasa ya mchepuo wa sayansi, Dar es Salaam Girl’s, iliyogharimu takriban zaidi ya sh. bilioni nne, huku mwasisi wa Shule hiyo akiwa yeye mwenyewe.
UTATUZI WA KERO NA CHANGAMOTO
Kero na changamoto nyingi zilitatuliwa kupitia mikutano ya hadhara iliyofanyika wakati wa ziara hiyo, ambapo kati ya kero hizo ni pamoja na Sekta ya ardhi, fidia za wananchi, maji, elimu, nishati ya umeme, miundombinu ya barabara na afya.
CPA Makalla akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shule ya Msingi Liwiti, alitatua kero ya wakazi wa Kipunguni, baada ya Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, kulalamikia juu ya wananchi wake wa Pingunguni kutolipwa fidia, baada ya kubomolewa nyumba zao kupisha upanuzi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA) Terminal 3 kwa takriban zaidi ya miaka 10.
Akitatua kero hiyo kwa njia ya simu mbele ya hadhara ya wananchi waliofika katika mkutano huo, CPA Makalla alizungumza na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba na kumtaka kutolea ufafanuzi suala hilo, ambapo alitoa ahadi kwamba wakazi hao wa Kipunguni wataanza kulipwa Agosti, 2024, huku aliomba radhi kucheleweshwa kwa ulipaji wa fidia hizo ulitokana na kuanza kwa mwaka mpya wa fedha.
Kero nyingine alizotatua akiwa katika mikutano yake ya hadhara ni kumtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Zaituni Hamza, kufuatilia suala la wananchi kulalamikia mwenendo mbovu wa wauguzi wa Hospitali ya Nguvu Kazi iliyopo Chanika, kuwatoza fedha wazazi pindi wanapoenda kujifungua na kuwapeleka watoto kliniki. Hivi karibuni Mwandishi wa Makala hii alifanya mawasiliano na Mganga Mkuu huyo na kueleza tayari changamoto hiyo imetatuliwa.
MATOKEO YA ZIARA
Ili kupata matokeo ya kufanyika kwa ziara hiyo, Mwandishi wa Makala hii aliwatafuta baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali, kusikia maoni yao kuhusu ziara hiyo na matokeo waliyopata.
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kinondoni, Shaweji Mkumbula, ameeleza baada ya kufanyika kwa ziara hiyo, kumewezesha kuwepo kwa hali ya uwamsho wa kisiasa katika wilaya hiyo tofauti na iliyokuwa awali.
“Kwa kweli tunashukuru sana kwa ujio wa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa na Mlezi wetu wa Chama kwa Mkoa huu wa Dar es Salaam, CPA Amos Makalla, kwanza kutokana na ziara yake kumetufanya kuwa na mwamko wa kisiasa, kero na changamoto nyingi za wananchi kwa kiwango kikubwa zimetatuliwa na pia, ametuongezea wanachama 600 kutoka vyama vya upinzani waliohamia CCM, hivyo tunashukuru na tunaomba ziara hizi ziwe endelevu” amesema Mkumbula.
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Ilala, Said Side, amesema: “Sisi kama wana Ilala tunasema ziara ilituletea hamasa ya kisiasa katika maeneo yetu hususan yale tuliyotembelea. Pia imeendelea kuhamasisha viongozi kuwafikia wananchi kusikiliza na kutatua kero zao kwa wakati na mwisho imetuongezea wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani.”
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameelezea matokeo chanya ya ziara hiyo kuwa ni kuendelea kukipa uhai Chama na kuendelea kujenga imani kwa wananchi kwa kuwa kero na changamoto zao zimetatuliwa na utekelezaji wa Ilani 2020/2025 umeendelea.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela Judith Ferdinand
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika