Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo tayari kushirikiana na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi katika kuendeleza uchumi wa visiwa hivyo, huku ikitaja sera ya uchumi wa buluu kama mhimili mkuu wa fursa mpya za kiuchumi.
Akizungumza katika jukwaa la uwekezaji lililowakutanisha wawekezaji kutoka zaidi ya nchi 20 za Afrika na nje ya bara hilo, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Omary Said Shaban, alieleza kuwa Zanzibar iko tayari kufanya maboresho ya sheria, kanuni na mifumo ya kibiashara ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
“Tunataka mazingira yawe rafiki kwa mwekezaji na kwa taifa. Tupo tayari kushughulikia changamoto za kisheria, kiutendaji na miundombinu kwa lengo la kuhakikisha wawekezaji wanapata kila hitaji muhimu la kuendesha shughuli zao kwa ufanisi,” amesema Waziri Shaban.
Ameipongeza benki ya Equity kwa hatua yake ya kuwaleta wawekezaji Zanzibar na kuunganisha visiwa hivyo na dunia ya uwekezaji. “Ni nadra kuona taasisi za kifedha zikichukua hatua ya moja kwa moja kuwasogezea wawekezaji fursa. Equity imeonesha kuwa iko mstari wa mbele katika kutekeleza wito wa Rais wa Zanzibar wa kuimarisha uwekezaji na biashara,” ameongeza.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Rashid Ali Salim, amesema jukwaa hilo limekuwa jukwaa muhimu kwa Zanzibar kueleza sera zake na fursa zilizopo, hususan katika sekta ya uchumi wa buluu inayojumuisha utalii wa baharini, uvuvi, usafirishaji wa majini, na bandari.
Ameomba benki ya Equity kuzingatia utoaji wa huduma za kifedha zinazofuata misingi ya Kiislamu ili kuwahudumia watu wasioweza kukopa kwa njia ya kawaida kupitia mfumo wa benki wa Kiislamu.

Mkurugenzi wa Biashara wa Equity Bank Tanzania, Prosper Nambaya, amesema benki hiyo itaendelea kuwa kiunganishi muhimu kwa wafanyabiashara wa Zanzibar kwa kuwawezesha kupitia mikutano ya ana kwa ana (B2B), mitaji, ushauri wa kiufundi, na kuangazia sekta zenye fursa kama kilimo, viwanda, vifaa na miundombinu.
“Benki ya Equity kupitia taasisi yake ya Equity Group Foundation inawekeza kwa dhati katika kuwainua wanawake, vijana na biashara changa. Tunaamini kwamba uchumi wa buluu ni eneo lenye nafasi kubwa kwa wawekezaji na tutahakikisha fursa zilizopo zinawafikia wanaostahili,” amesema Nambaya.

Kwa mujibu wa benki hiyo, Equity ina mtaji wa takriban dola bilioni 2 na mizania ya zaidi ya dola bilioni 14. Ina uwezo wa kufadhili miradi mikubwa hadi dola milioni 5 kwa mradi mmoja, hali inayoongeza imani kwa wawekezaji kuwa wanaweza kuwekeza Zanzibar bila mashaka.
Kavsel Kocadag, mmoja wa washiriki wa jukwaa hilo, ameeleza kuwa fursa zilizopo Zanzibar ni muhimu kwa ukuaji wa biashara barani Afrika na kimataifa, akibainisha kuwa mikutano kama hiyo ni njia bora ya kutangaza vivutio na fursa za kiuwekezaji zilizopo visiwani humo.

Kwa upande wake, Rahim Khaji Hamza, Meneja wa Uwekezaji kutoka Shirika la Bima Zanzibar, amesema jukwaa hilo limewapa nafasi ya kuonesha namna ambavyo wanaweza kutoa huduma za bima kwa wawekezaji, na kulinda miradi yao dhidi ya hatari mbalimbali.
Kwa ujumla, jukwaa hilo limeonesha dhamira ya pamoja kati ya sekta binafsi na serikali katika kuimarisha Zanzibar kama kitovu cha kiuwekezaji, kikijikita katika matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa maendeleo ya uchumi wa visiwa hivyo.
More Stories
Mwongozo wa kitaifa kwa watoa huduma za maendeleo ya biashara wazinduliwa
Elimu ya kilimo tija yawafikia wakulima mikoa mitano.
DCEA yateketeza ekari 157 mashamba ya bangi Kondoa