March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya wanawake 500,wapatiwa ujuzi mbalimbali Tabora

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora

WANAWAKE zaidi ya 500 mkoani Tabora,wamepatiwa ujuzi katika fani mbalimbali ambao utakuwa kichocheo cha kuanzisha miradi na kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia mkoani Tabora,Josephine Mbaga,wakati akizungumza na wanawake zaidi ya 1000 walioshiriki mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Amesema wanawake hao walipatiwa mafunzo ya ujuzi mbalimbali na chuo cha VETA,kupitia Taasisi ya Wanawake na Samia, ikiwemo ushonaji, mapishi, ususi, saluni, utengenezaji batiki, ufundi umeme wa nyumbani, udereva wa magari, usafi na mapambo.

‘Mafunzo haya hutolewa bure ni kichocheo muhimu kwa wanawake kuanzisha miradi yao wenyewe,ambayo itawasaidia kuingiza kipato na sio kuendelea kuwa tegemezi kwa waume zao,”amesema Mbaga.

Pia ametoa rai kwa wanawake waliopata na wanaoendelea kupata mafunzo hayo kutokaa nyumbani bali watumie ujuzi waliopata kama fursa muhimu ya kuwaingizia kipato.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora Upendo Wella, Kaimu Ofisa Tarafa na Mtendaji wa Kata ya Tambukareli,Hussein Hamis, amepongeza Taasisi ya Wanawake na Samia kwa mikakati yao kuinua wanawake huku akiwasisitiza wanufaika kutumia fursa ya mafunzo hayo kukikomboa kiuchumi.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono na kuwapa ushirikiano unaotakiwa ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao kupitia mafunzo hayo.