Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Ukerewe
Zaidi ya wakazi 6000 wa kisiwa cha Gana kilichopo wilayani Ukerewe mkoani Mwanza wanatarajia kunufaika na huduma za usalama baada ya mfanyabiashara na mkazi wa Kata ya Ilangala kisiwani humo analifahamika kwa jina la Nyamitere Ugunya kutoa nyumba yake ili iwe kituo cha polisi.
Nyumba hiyo yenye vyumba zaidi ya 15 inatakiwa kufanyiwa ukarabati mdogo wa kuwekewa miundombinu na mifumo ya majitaka itakayokidhi hadhi ya kituo cha polisi.
Akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo hilo kunaenda kutatua changamoto za kiusalama ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi kisiwani humo.
Sanjari na hayo ametumia fursa hiyo kumuomba mfanyabiashara huyo aliyejitolea kujenga kituo cha polisi kukamilisha mapema hadi ifikapo mwishoni mwa Januari 2024.
“Niwapongeze wananchi wa eneo hili kwa kukubali kujenga kituo cha polisi katika eneo hilo, ikiwezekana kabla ya mwisho wa mwezi Januari 2024, kiwe kimekamilika na mimi nitatamani kukizindua ili tuweke askari wa kutosha na kuanza kufanya kazi,” amesema Kamanda Mutafungwa.
Hata hivyo, wakazi wa Kisiwa hicho wamemweleza Kamanda Mutafungwa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo na kuomba Serikali iwatatulie ikiwa ni kukithiri kwa vitendo vya mmonyoko wa maadili, ulevi, utovu wa nidhamu, wizi wa nyavu na injini za mitumbwi, uvuvi haramu, ukatili wa kijinsia, udokozi, mauaji, unyanyasaji na ukosefu wa alama za mipaka ziwani zinazoonyesha mpaka wa Tanzania na Uganda.
Kwa upande wao wananchi wa kisiwa hicho wameliomba Jeshi la Polisi kusaidia kukamilisha mapema ujenzi wa kituo hicho ili changamoto zitatuliwe huku wakiomba mipaka inayotenganisha Tanzania na Uganda iwekwe ziwani ili kupunguza matukio ya wavuvi wa pande hizo mbili kuingiliana.
Mmoja wa wavuvi kisiwani hapo Swai Somba, amemwomba Kamanda Mutafungwa kuharakisha ujenzi wa kituo hicho cha Polisi kutokana na changamoto ambazo wananchi wa eneo hilo zaidi ya 6,000 wamekuwa wakikumbana nazo.
“Tunapotoka hapa kisiwani kuingia ziwani kuvua tunanyanyasika kutokana na vyombo vyetu mfano sisi wavuvi wa kasia uvuvi wetu ni duni lakini wanaotumia mashine wametuwekea masharti ambayo mimi ninashindwa kujua moja wapo ukitoka ziwani ukileta hapa samaki unaanza kuulizwa umetumia zana gani kuvua wakati huenda ulikuwa na ndoano, tunaomba msaada katika hili,”amesema Somba.
Naye Kemelo Matiku,amehoji ni lini watawekewa mipaka ziwani kwani wamekuwa wakisumbuliwa na wavuvi na Askari wa Uganda ambao wamekuwa wakiwakamata na wakati mwingine kuwanyang’anya nyavu na samaki zao.
Akijibu swali hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri na Uvuvi Endelevu Ziwa Victoria, Bakari Kadabi amesema, kuanzia Januari 2024 Serikali inatarajia kuweka mipaka ziwani itakayokuwa inawasaidia wavuvi kujua upande wa Tanzania na Uganda.
“Serikali imejipanga kuanzia mwezi Januari kuweka maboya mpakani kati ya Tanzania na nchi jirani kwa hiyo tatizo la kuingilia linaenda kuisha kabisa ila niwaombe wavuvi muwe wakweli hamna sababu ya kwenda kuvua upande wa Uganda wakati huku tuna maeneo mengi ya kuvua,” amesisitiza Kadabi.
Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa ametangaza kufanya oparesheni kabambe na endelevu ndani ya Ziwa Victoria na maeneo mengine ili kutokomeza uhalifu na kuimarisha ulinzi na usalama zaidi katika maeneo yote.
More Stories
Simbachawene:Waombaji wa ajira jiungeni na Mfumo wa Ajira Portal
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki