Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Magu
Serikali imetenga zaidi ya milioni 600, kwa ajili ya kupeleka huduma ya nishati ya umeme wa jua,kwa wananchi wa Kisiwa cha Ijinga,kilichopo wilayani Magu mkoani Mwanza.
Kisiwa hicho ambacho ni pekee katika Wilaya ya Magu ambacho hakina huduma ya nishati ya umeme kati ya vijiji 82,,vilivyopo wilayani humo.
Hayo yamebainishwa Desemba 23,2024, na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakati akihutubia wananchi katika mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Magu,ambao Mbunge wa Jimbo la Magu Boniventura Kiswaga aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa miaka minne(2020-2024),ambapo amesema
Mkandarasi wa mradi huo kampuni ya Master Volt Ltd yupo eneo hilo kwa ajili ya kupeleka umeme Jua (Solar).
“Mnavijiji 82, vijiji 81 vyote vina umeme kimebaki kijiji kimoja,ambacho ni kisiwa, tuliona itachukua muda kuwapelekea umeme kwa kulaza nyaya kwenye maji,kwani watu wa Ijinga ni Watanzania wanastahili kupata umeme tumetenga milioni 619 ili nao wapate umeme,” amesema Biteko.
Kwa upande wake Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga amesema,kazi kubwa imefanyika asilimia 99 ya vijiji vilivyopo jimboni humo vimepata umeme,kimebaki kijiji kimoja tu cha Ijinga,vijiji 81 tayari vyote vina umeme kati ya vijiji 82.
Sanjari na hayo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo inakwenda kuokoa mazingira na afya za wananchi.
“Naipongeza REA kwa kuibeba ajenda hii ya Rais, kwa kuandaa programu mbalimbali ikiwemo ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya 50%,” amesema Kiswaga.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini, Msimamizi wa Miradi Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Awesa Rashid, amesema REA inatekeleza miradi mbalimbali mkoani humo,baada ya kukamilisha kusambaza umeme vijijini na sasa ni zamu ya vitongoji.
“Tunatekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 15 kwa kila Jimbo ikiwemo la Magu, ambapo kwa sasa mradi huu unaendelea,”amesema Awesa.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa bei ya shilingi 27,000 tu ili kujiletea maendeleo.
Aidha, akizungumzia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Ramadhani Mganga,amesema REA inaendelea kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa za nishati safi za kupikia ili kuepukana adha mbalimbali zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi.
“Tumuunge mkono Rais Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034,”amesema Mhandisi Mganga.
Mhandisi Mganga,amesema kwa upande wa Mkoa wa Mwanza jumla ya majiko 19,530 yatasambazwa ambapo kila wilaya itapata majiko 3,255 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 huku akisisitiza wananchi wanapokwenda kununua mtungi huo wa ruzuku ni lazima uwe na kitambulisho cha Taifa.
“Mpango huu wa Serikali tumeupokea vizuri. Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani ameturahisishia sisi watanzania tulikuwa tunakata miti ovyo ili kupata kuni na mkaa, na sasa madhara yake tunayaona,”amesema Sebastian Boniphace Mkazi wa Magu.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni