January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya milioni 50 zatolewa kutengeneza madawati

Na George Mwigulu,Timesmajira Online,Katavi

Kampuni ya ununuzi wa tumbaku ya Premium Active Tanzania imetoa msaaada wa zaidi ya milioni 50 kwa ajili ya sekta ya elimu zitakazotumika kutengeneza madawati kwa shule za msingi na sekondari mkoani Katavi.

Hundi ya fedha hizo imekabidhiwa kwa Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Onesmo Busweru ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika na Meneja shughuli wa hampuni hiyo Nico Rousss kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika .

Akikabidhi mfano wa hundi hiyo Rousss amesema kampuni hiyo imetoa kiasi hicho cha fedha ambazo zitagawiwa kwenye maeneo ya Kata zote zinazolima tumbaku ikiwa ni sehemu ya kuchangia maendeleo katika maeneo yote yanayolima zao Mkoa wa Katavi .

Amebainisha kuwa kampuni hiyo licha ya kununua tumbaku wao ni sehemu kubwa ya wadau wa kuleta maendeleo katika Mkoa wa Katavi na ndio maana wameamua kutoa kiasi cha 50,300,000 katika sekta ya elimu kwa ajili ya kutengeneza madawati ya shule za msingi na sekondari .

Katika kufanikisha mchango huu kwenye jamii walipokea maombi ya miradi mbalimbali ya kipaumbele kwenye kila Kata kutoka vyama vya ushirika vya Msingi vinavyofanya kazi na kampuni hiyo kwa hali hiyo sio rahisi kwa sasa kutimiza miradi hiyo kwa wakati mmoja .

“Kati ya fedha tuluzotoa kiasi cha zaidi ya milioni 31 ni kwa ajili ya Wilaya ya Tanganyika,Wilaya ya Mpanda milioni 11.25 na Wilaya ya Mlele milioni 7.22 hivyo kampuni inayofuraha kubwa ya kuwa wadau waliorudisha faida yao kwenye maendeleo ya jamii.

Meneja Uhusiano na Usimamizi wa kampuni hiyo Yusuph Mahundi amesema kampuni inafanya kazi katika maeneo yote ya Mkoa wa Katavi huku Wilaya ya Tanganyika ndiko wanakofanya kazi kwa sehemu kubwa.

Msimu wa kilimo uliopita wamefanya kazi katika vyama vya msingi 14 na kati vyama hivyo walitowa malengo ya uzalishaji kili milioni 11.6 lakini ilipofika mwisho wa msimu waliweza kununua kilo milioni 8.3 ambazo ndio zilikuwa zimezalishwa .

Ambazo kwa ujumla wake zilkuwa na thamani ya dola 19.7 kwa fedha za kitanzania ni sawa na bilioni 47.4 ambapo kwenye fedha hizo kiasi cha Dola 500,000 waliweza kulipa ushuru kwenye Halmashauri za maeneo yanayolima tumbaku ambazo ni sawa na fedha za Kitanzania zaidi ya bilioni 1.4 .

Mahundi ameeleza kuwa wanaamini kiwango hicho cha fedha ni kikubwa ambacho kinaweza kuleta chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi na pia kwa Halmashauri za Mkoa wa huo.

Ameeleza kwa msimu ujao wa kilimo Kampuni hiyo inatarajia kununua kilo za Tumbaku milioni 11. 7 ambapo wameweza kuingia mikataba na vyama 16 vya ushirika vya msingi.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini Moshi Kakoso amesema kiasi hicho cha fedha kilichopokelewa kitatumiwa vizuri kwenye maeneo yote ya Halmashauri za Mkoa wa Katavi .

Ameiomba kampuni hiyo isiwachoke pindi watakapokuwa wamewaomba tena msaada kama huu kwa ajili ya huduma kwenye sekta nyingine kwani yeye anatambua kuwa kampuni hiyo ni kubwa hapa Duniani kwani inashika nafasi ya tatu kwa ukubwa kati ya kampuni yanayo nunua tumbaku .

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ameishukuru kampuni hiyo kwa kuweza kuguswa na kile walichoweza kupata kama faida yao na kisha sehemu kuirudisha kwa wananchi kwenye kufanya shughuli za maendeleo katika sekta ya elimu .

Amesisitiza kuwa Halmashauri zote zilizopata fedha hizo kwa ajili ya kutengeneza madawati zihakikishe ifikapo Desemba 31 ziwe zimekamilisha utengenezaji wa madawati hayo na wazingatie yawe na ubora ili watoto wa wakulima wa tumbaku na wasio wakulima kuweza kuyatumia .