January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya milioni 123 za TASAF kujenga jengo la upasuaji zahanati ya Mahina

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

DIWANI wa Kata ya Mahina (CCM),Alphonce Francis amesema mradi wa jengo la upasuaji la zahanati ya Mahina unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa zaidi ya milioni 123,utatatua changamoto ya huduma hiyo kwa wananchi wa kata hiyo.

Francis amesema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi,leo wakati akifungua mafunzo kwa Wajumbe wa Serikali ya Mtaa na Kamati ya Usimamizi wa mradi huo kutoka mitaa ya Kagomu na Igelegele.

Amesema mradi huo unaotekelezwa katika zahanati ya Mahina utaondoa changamoto ya tiba ya upasuaji kwa wakazi wa Kata hiyo utakapokamilika huku ameipongeza serikali kwa kuboresha huduma za afya ikiwemo kujenga miundombinu, kununua dawa,vifaa tiba na vitendanishi hivyo wananchi waiunge mkono.

Ameeleza mradi wa jengo la upasuaji unaokwenda sambamba na mradi wa OPD ambao umefikia asilimia 80,utaiwezesha zahanati ya Mahina kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya chenye vifaa vya kisasa itakapokamilika hivyo jamii ishiriki kuchangia asilimia 10 ya nguvu kazi yao sawa na milioni 8 mradi huo ukamilike na kuwapa manufaa.

“Tushiriki na kuiunga mkono serikali inayogharamia asilimia 90 ya mradi na jamii asilimia 10,mnataka viongozi mliowachagua wawaletee nini,furahini kupata mradi wa zaidi ya milioni 121 lakini msiwe sehemu ya hujuma ya mradi huu ni mali yenu tuufanye tuandike historia,”amesema Francis.

Diwani huyo wa Mahina amesema,hatakuwa radhi na hatakubali kuona mradi huo unakwama au unaondolewa sababu ya usimamizi na kusistiza kuwa ni lazima watu wachache waumie kwa manufaa ya wengine na vizazi vijavyo ikizingatiwa miradi wanayoitumia watu waliwajibika kuifanya wakaacha alama.

Katibu wa CCM Kata ya Mahina, Vitalis Makorosho amewataka wasimamizi wa mradi huo wa kimkakati kujitoa kuusimamia kwa weledi ulete manufaa na kuonesha imani kwa jamii iliyowachagua kuusimamia.

“Maendeleo hayaji bila kujitoa,tukijitoa na kuukamilisha thamani ya fedha ikaonekana hata waliotuletea mradi huo wa jinge la upasuaji watafarijika,”amesema na kuongeza kuwa katika usimamizi wa maslahi ya watu halazi damu na hana mzaha.

Naye mkazi wa Igelegele na mmoja wasimamizi wa mradi huo wa jengo la upasuaji,Zihaya Khalid, ameahidi kutumia elimu na alichojifunza kuwaelimisha wananchi au jamii faida na manufaa ya mradi hasa akinamama ambao ni wanufaika wakubwa wanapopata changamoto ya kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Sisi akinamama lazima tujivune kupata mradi huu sababu utakuwa na manufaa kwetu kuliko watu wengine,hivyo nitawajibika kuwaelimisha wanaodhani mradi hauna maslahi kwao na kuwahamasisha kujitolea ili ukamilike,”amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Jiji la Mwanza, Peter Ngagani ameeleza kuwa serikali imewekeza kiasi cha milioni 123.7 katika mradi huo wa afya na mfuko huo umejipanga kufanya mikutano ya kuhamasisha jamii inayonufaika ishiriki kuchangia nguvu kazi yao ama fedha ili kukamilisha asilimia 10.