Na Yusuph Mussa,TimesMajira Online, Lushoto
Miche ya kahawa 227,905,imetolewa bure kwa wakulima wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ikiwa ni jitihada za kuweza kurejesha tena zao hilo ambalo lilishamiri zaidi ya miaka 50 iliyopita kwenye wilaya hiyo.Jitihada za kurejesha zao hilo linafanywa na Bodi ya Kahawa Tanzania, Kanda ya Kaskazini ili kuwawezesha wataalamu wa kilimo kwenye halmashauri ikiwa ni pamoja na kugawa miche na kutoa mafunzo kwa maofisa ugani na wakulima.
Uzinduzi wa kugawa miche ya kahawa umefanyika Mei 9, 2023, kwenye kitalu cha miche hiyo kilichopo eneo la Jegestali mjini Lushoto, huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro ambaye amezungumza na wakulima hao waliotoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushiriki zoezi la kugawa miche kwa wakulima, Lazaro amesema zao la kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati kwenye wilaya hiyo, hivyo wanataka kurudisha kilimo hicho kama ilivyokuwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Amesema kazi yao viongozi wa Wilaya ya Lushoto ni kuona wakulima wao wanakuwa na mazao ya kimkakati hasa ukichukulia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka nguvu nyingi kwenye kilimo.
Ambapo mwaka jana Bodi ya Kahawa Tanzania, Kanda ya Kaskazini iligawa miche 68,000 kwa wakulima wao, lakini wakaona hiyo haitoshi, ni vizuri Lushoto ikawa na kitalu cha miche hivyo wamepanda miche 300,000 na siku hiyo wakulima wamewagawia miche 227,905.
“Tunataka kuliendeleza zao la kahawa kama ilivyokuwa siku za nyuma, na zao hili ni la kimkakati,Wilaya ya Lushoto ina mazao ya kimkakati matano ambayo ni kahawa, mkonge kule chini eneo la tambarare, parachichi, ngano na chai kule Bumbuli kwa mazao hayo, wakulima wetu watakuwa na uhakika wa kipato,”amesema Lazaro.
Naye Ofisa Maendeleo wa Kahawa Kanda ya Kaskazini Saidi Ng’ombo,amesema, Bodi ya Kahawa Tanzania imeweka malengo ya kufikisha uzalishaji wa tani 300,000 za kahawa safi ifikapo mwaka 2025, hivyo katika kufika lengo hilo katika msimu wa 2022/23, iliweka lengo la kuzalisha miche 2,000,000 katika Kanda ya Kaskazini na kuigawa kwa wakulima wa kanda hiyo.
“Katika kutekekeleza adhima hii na ikiwa Lushoto ni miongoni mwa Wilaya zinazozalisha kahawa kwa kiwango cha chini, na kwa kuzingatia mapendekezo ya Mbunge wa Mlalo Rashid Shangazi, bodi imeanzisha kitalu cha miche ya kahawa kilichopo maeneo ya Jegestali, Lushoto mjini chenye uwezo wa kuzalisha miche 300,000 lakini bodi mpaka sasa imeshazalisha miche 227,905 ambayo iko tayari kwenda shambani kipindi hiki cha masika,”amesema.
Aidha amesema miche hiyo inatarajia kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 50 hadi 75 kwa mwaka kwa msimu wa 2020/21 na 2021/22.
“Kwa misimu ya nyuma wilaya hii ilikua ikizalisha tani 250 kwa mwaka matarajio yetu ni kufika tani 500 kwa mwaka ifikapo 2025/26, ambapo itachangia kuongeza kwa ukuaji wa uchumi kwa wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Halmashauri ya Bumbuli, na hata kuongeza mapato kwa halmashauri hizi,”amesema Ng’ombo.
Kaimu Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto George Medeye amesema miche 227,905 iliyogawiwa ina uwezo wa kupandwa kwenye eneo la hekari 228.
Huku akisisitiza kuwa uwezeshwaji wote unaofanyika kwa ajili ya kuinua tena kilimo cha kahawa wilayani humo, unafanywa na Bodi ya Kahawa Tanzania, Kanda ya Kaskazini.
More Stories
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi
Rais Samia apongezwa kwa miongozo madhubuti ya ukusanyaji wa kodi
Mwenda:Siku ya shukrani kwa mlipakodi ni maalum kwaajili ya kuwatambua,kuwashukuru