November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya Kampuni 1000 kushiriki maonesho ya 47 ya biashara nchini

Na David John Timesmajira online

KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya ukuzaji biashara kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade Fortunatus Mhambe Amesema kuwa kampuni 1188 kutoka hapa nchini na 112 kutoka nje ya nchi zimethibitisha kushiriki maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya sabasaba yanayotarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Leo Mei 19 kwenye ofisi za Mamlaka zilizopo kwenye viwanja vya Sabasaba vya Mwalimu Nyerere barabara ya kilwa wilayani Temeke .

Mhambe amesema mpaka sasa nchi takribani 14 ikiwemo China na Umoja wa Falme za Kiaràbu zimethibitisha kushiriki katika maonesho hayo yenye kauli mbiu “Tanzania, mahali sahihi pa biashara na uwekezaji “

“lengo kuu la maonesho haya ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi na kuwapa fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kutafuta masoko mbalimbali.

Nakuongeza kuwa “Maonesho ya 47 ya biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yatakuwa na maeneo mbalimbali yaliyoboreshwa na programu za kuvutia ikiwemo ya Sabasaba Expo Village, ili ni eneo ambalo limetolewa kutangaza fursa zilizopo katika sekta ya madini, Tehama, gesi na mafuta, siku ya mazingira, sanaa, vijana pamoja na wanawake,” amesema

Mhambe ametoa wito kwa wafanyabiashara kushiriki katika maonesho hayo ya 47 pamoja na kutembelea banda maalum la Sabasaba Expo Village ili kuchangamkia fursa zilizopo na kuongeza kuwa hiyo ni nafasi nzuri kwa wajasiriamali kukuza na kujenga mtandao wa kuinua biashara zao.

“Hata hivyo Sabasaba Expo Village inatoa jukwaa la kujenga mtandao wa kibiashara kwa wafanyabiashara na kuwapa fursa ya kuanzisha mawasiliano na wenzao, kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano mpya, eneo hili litawavutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo wawekezaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa biashara,” amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza amesema wataendelea kuwawezesha wanawake kushiriki katika maonesho hayo ambayo yamekuwa ni chachu kubwa kwa washiriki wengi hasa kupata masoko ya uhakika.

“Maonesho haya yamesaidia wajasiriamali wetu kupata masoko ya uhakika, hivyo ushiriki ni mkubwa na tunawaahidi TanTrade kuwa tutaendelea kuyatangaza maonesho haya ambayo yanatoa fursa ya watu kujitangaza na kuuza biashara zao kwa viwango wa hali ya juu,” amesema

Naye kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mwanakhamis Hussein amesema wataendelea kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kushiriki maonesho hayo na fursa gani wanaweza kuzipata kwa lengo la kuinua biashara zao.