January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya bilioni 22 kujenga barabara Mwanza

Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Mwanza.

SERIKALI imetoa zaidi ya bilioni 22 katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 14 kwa kiwango cha lami kutoka Buhongwa kwenda Igoma ikiwa ni hatua ya ya utekelezaji wa mipango mikubwa ya ujenzi wa barabara jijini humo.

Shughuli hiyo inatekelezwa na kampuni ya kichina ya Zhongmei Group na inatarajiwa kukamilika kwa wakati.

Pamoja na mpango huo Halmashauri ya Jiji la Mwanza pia linatarajia kukarabati barabara zote zilizoharibiwa na mvua mara baada ya mvua kupungua.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Jiji hilo Aroun Kagurumjuli Februari 15,mwaka huu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea ofisini kwake.

Kagurumjuli amesema pamoja na shughuli za ujenzi wa barabara pia Jiji hilo limepokewa fedha kiasi cha bilioni 3.4 kwa mwaka wa fedha 23/24 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kukidhi mapungufu ya vyumba katika shule za sekondari .

“Tunampongeza Rais wetu kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwezesha huduma za kijamii katika eneo letu kwani hatua hiyo ni muhimu katika jiji letu linaloendelea kukua kila siku,”amesema Kagurumjuli.

Amesema vilevile Jiji hilo limepokea milioni 400 kwa ajili ujenzi wa shule mpya maalum ya sekondari katika eneo lenye uhitaji mkubwa wa shule hizo.

Kagurumjuli amefafanua kuwa ujenzi wa shule hizo zinatarajia kukamilika kwa wakati ili ziweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Julai mwaka huu.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa Jiji hilo limetangaza tenda kwa ajili ya ujenzi wa soko la Kimataifa la samaki kwa kasi kubwa katika eneo la Mkuyuni ili liweze kuanza kutoa huduma zake mapema kutokana na uhitaji wake kwa wafanyabiashara.