March 3, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya bilioni 1.1 kunufaisha vikundi 60 Ilemela

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

JUMLA ya bilioni 1.135 za mikopo isiyo na riba imetolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa vikundi 60 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu,ili kuwawezesha kiuchumi na kuboresho ustawi wa maisha yao.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela, Mariamu Msengi, amekabidhi mikopo hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Hassan Masalla, na amesisitiza kuwa itumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuboresha hali za kiuchumi na maisha ya wanufaika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ummy Wayayu,amesema vikundi 60 vilichaguliwa kutoka kwenye maombi 216 yakiomba bilioni 9, ambapo vikundi 39 vya wanawake vitapata jumla ya milioni 618, vikundi 17 vya vijana milioni 492,na walemavu milioni 24.

Amesisitiza umuhimu wa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili wengine pia wapate fursa ya kukopa.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga, ameonya wanufaika kutokukimbia kurejesha fedha za Serikali, huku akisisitiza kuwa fedha hizo zitasaidia maendeleo ya jamii.

Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo,Yohana Matahe,ameahidi kutumia fedha hizo vizuri na kurejesha kwa wakati.

Spesioza Alex, kutoka kikundi cha Balimi Basukuma,ameahidi watakuwa mfano kwa wengine kurejesha mkopo huo na kuiomba Serikali kuvifuatilia mara kwa mara ili vikundi hivyo vitumie fedha hizo kwa manufaa na kutatua changamoto zinazojitokeza