March 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi 2000 kushiriki ‘Lake Zone International Marathon’

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

Zaidi ya washiriki 2000 wanatarajiwa kushirki katika mbio za Kimataifa za Utalii Kanda ya Ziwa 2025 (Lake Zone International Marathon 2025) zitakazofanyika mkoani Mwanza Juni 27 hadi Juni 29,2025,zenye lengo la kuhamasisha utalii na kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo.


Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Kilimanjaro One Sports Promotion Ltd, Mohamed Hatibu, amesema mbio hizo ambazo zitafanyka mkoani Mwanza zitaambatàna na tamasha la utamaduni linalotarajiwa kufanyika mkoani Simiyu.

Amesema kuwa lengo la mbio hizo ni kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, ili kuchangia katika kukuza uchumi wa mkoa na taifa zima.


“Vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji Kanda ya Ziwa ni vingi,ni muhimu Watanzania kuvitangaza ili kuvutia wageni na kuingiza fedha za kigeni zinazosaidia maendeleo ya sekta mbalimbali,” amesema Hatibu.

Amesema,mbio hizo zitahusisha makundi mbalimbali, wakiwemo wajawazito, watoto, walemavu, wazee na viongozi kutoka Mikoa mbalimbali.Pia wananchi watahamasishwa kushiriki katika uchaguzi mkuu mwaka huu kwa amani.

Rhoda Kabarua, Msimamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, amesema kwa kushirikiana na Kilimanjaro One Sports Promotion, mbio hizo zitakuwa ni makakati wa kutangaza vivutio vya utalii vya Mwanza ikiwemo Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane na Makumbusho ya Utamaduni wa Wasukuma Bujora.

Amesema michezo hutoa fursa ya kukutanisha watu kutoka sehemu mbalimbali, hivyo mbio hizo zitakuwa na manufaa kiuchumi na zitaongeza mapato ya mkoa kupitia utalii.

Kwa upande wake, Bertha Nikundiwe, Mtaribu wa Huduma ya Afya ya Uzazi, Jiji la Mwanza, amesema mbio hizo pia zitatoa nafasi ya kutoa elimu ya afya ya wajawazito na umuhimu wa mazoezi katika kupunguza vifo vya watoto wachanga na wajawazito.

Amesema wajawazito watashiriki kwa kutembea kwa dakika 20 hadi 30 na kufanya mazoezi mepesi, ambayo yanafaida kwa afya zao, ikiwemo kuboresha mzunguko wa damu na kupunguza shinikizo la damu, sukari na kupunguza uzito, huku akisisitiza licha ya faida hizo, wanawake wenye matatizo ya kiafya yanayohusiana na mimba hawataruhusiwa kushiriki.