Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.
WANANCHI wa Kijiji cha Nyabaengere Kata ya Musanja Wilaya ya Musoma Mkoani Mara, wameanza kunufaika na Huduma za Afya ambazo zimeanza kutolewa katika Zahanati ya Kijiji chao na hivyo kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda kupata Huduma hizo kwenye Kata Jirani ya Murangi.
Ujenzi wa Zahanati hiyo umehusisha Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospter Muhongo, michango ya fedha za Wananchi na nguvu kazi zao, Viongozi wa kata, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na fedha kutoka serikali kuu.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Disemba 6, 2024,imeyabainisha hayo na kuongeza kuwa, Utoaji wa Huduma za Afya umeendelea kuboreshwa ndani ya vijiji vya Jimbo hilo na kuwapa uhakika wa Huduma za Afya Wananchi.
“Kata ya Musanja yenye vijiji vitatu (Mabuimerafuru, Musanja na
na Nyabaengere. Vijiji viwili (Nyabaengere na Mabuimerafuru) vinajenga zahanati za vijiji vyao. Na leo Kijiji cha Nyabaengere kimezindua utoaji wa Huduma za Afya kwenye zahanati yake mpya.”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ujenzi wa Zahanati hiyo ulianza kupitia Harambee ya Mbunge wa Jimbo Prof. Sospter Muhongo kuchangia mifuko 100 ya Saruji, pia kwa kukusanya michango na nguvu kazi za wanakijiji na viongozi wao.
Pia, Diwani na Wanakijiji walichangia michango yao yenye takribani Shilingi Mil. 5, Wazaliwa wa Kijiji cha Nyabaengere nao wamechangia jumla ya Shilingi 400,000.
“Baadae, Halmashauri yetu (Musoma DC ) ilichangia Shilingi Mil. 50. Na
vilevile, Serikali Kuu ilichangia Mil. 50, huduma za afya zimeanza kutolewa. Huku ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu inayohitajika unaendelea.”imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Wananchi wa Kijiji hicho na Jimbo la Musoma Vijijini kwa ujumla, wameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuchangia fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya Maendeleo katika Vijiji mbalimbali jimboni humo.
“Nafurahi kuona Huduma za Afya zinatolewa kwenye Zahanati hii ambapo tutakuwa tunapata matibabu ya kawaida hapa hapa badala ya kutembea kwenda Murangi. Haya yote ni mageuzi makubwa sana ambayo tumeendele kuyapata jimboni mwetu yakichangiwa na uhodari wa Mbunge wetu Prof. Muhongo, pia Rais wetu Dakt. Samia Hassan ambaye amekuwa akitoa fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo.”amesema Mafuru Juma Mkazi wa Nyabaengere.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais