May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zahanati iliyounganishwa umeme wa REA yatakiwa kuanza kazi mara moja

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, kuhakikisha Zahanati ya Kijiji cha Mkangwe, iliyounganishiwa umeme wa REA inaanza kazi mara moja.

Ametoa maagizo hayo Februari 22, mwaka huu wakati akizungumza na wananchi baada ya kuwasha umeme katika Zahanati hiyo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko akikata utepe pamoja na viongozi mbalimbali kabla ya kuwasha Umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Mkangwe, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, Februari 22, 2024.
 

“Umeme tayari tumewasha, kwahivyo hakuna haja ya kusubiri. Naagiza Zahanati hii ianze kazi Jumatatu ijayo (Februari 26) ili wananchi wapate huduma za afya kama Serikali ilivyodhamiria,” amesisitiza.

Aidha, Dkt. Biteko amewaagiza Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati ili Serikali iendeleze miradi hiyo katika maeneo mengine ambayo hayajafikiwa.

Amesema, kadri miradi ya umeme vijijini inavyoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali, kiu ya wananchi ambao hawajafikiwa inaongezeka hivyo ameiagiza REA kuhakikisha inasimamia suala la ukamilishwaji miradi hiyo kwa wakati.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kwa Mkoa wa Iringa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema Vijiji vyote 360 vya Mkoa huo, sawa na asilimia 100 vimepatiwa huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko akiwasha umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Mkangwe, Wilaya ya Mufindi, Februari 22, 2024.

Ameongeza kuwa, mbali na kufikisha umeme katika vijiji vyote, REA pia imefikisha nishati hiyo katika vitongoji 1,188 kati ya 1,853 sawa na asilimia 64.11

“Vitongoji vilivyobaki vipo kwenye mpango wa kufikishiwa huduma ya umeme kupitia miradi ya ujazilizi na miradi ya vitongoji,” amesema Chibulunje.

Akitoa takwimu za Jimbo la Mufindi Kusini, ambapo ndipo kilipo kijiji cha Mkangwe, Mhandisi Chibulunje amesema vijiji vyake vyote 71 sawa na asilimia 100 vimekwishafikishiwa umeme kupitia miradi mbalimbali ya REA.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji pamoja na Mradi wa kupeleka umeme kwenye Vitongoji.

Mwonekano wa Zahanati ya Kijiji cha Mkangwe ambapo Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko aliwasha umeme Februari 22, 2024.

Kuhusu Vitongoji, ameeleza kuwa Jimbo la Mufindi Kusini lina jumla ya Vitongoji 305 ambapo kati yake, 191 tayari vimekwishapatiwa umeme.

Kwa upande wa gharama zilizotumika kutekeleza miradi ya umeme katika vijiji vya Jimbo la Mufindi Kusini, amesema kuwa jumla ya shilingi bilioni 7.6 zimetumika.

Hafla hiyo ya kuwasha umeme imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa na Serikali, wananchi pamoja na Wataalamu kutoka REA na TANESCO.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Godfrey Chibulunje akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Mkangwe, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, Februari 22, 2024.