November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

YoWDO yatoa mafunzo kwa wanahabari juu ya masuala ya watu wenye ulemavu

Na Penina Malundo

TAASISI ya Vijana Wenye Ulemavu (YoWDO), imetoa mafunzo kwa wanahabari juu ya masuala ya watu wenye ulemavu kwa lengo la  kuondoa  vikwazo vinavyosababisha kundi hilo lisishiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo ya Taifa  na kuhakikisha  jamii inaelimishwa juu ya  lugha sahihi ya kuwaita watu wenye ulemavu.

Akizungumza hayo jana  jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Programu wa YoWDO, Genarius Ernest wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya  watu wenye ulemavu, iliyoandaliwa na  taasisi hiyo.

Amesema elimu juu ya watu wenye ulemavu  inahitaji kuendelea kutolewa kwa kila hatua ili kuondoa mitazamo iliyopo katika jamii inayofikilia juu ya mitazamo.

Ernest amesema kuna aina tatu ya mitazamo kwa watu wenye ulemavu ikiwemo mtazamo wa kitabibu,mtazamo wa Kihisia na Mtazamo wa Kijamii ambapo watu wenye ulemavu ukumbwa na vikwazo  vya jamii.

Amesem asilimia kubwa ya watu  wenye ulemavu wanaachwa katika fursa za mbalimbali za kimaendeleo, kutokana na kuwekewa vikwazo ndani ya jamii kutokana na hali yao.

“Kumekuwa na mtizamo tofauti katika jamii kuona   watu wenye ulemavu hawawezi kufanya jambo lolote,hivyo wanakumbana na vikwazo vilivyotengenezwa na jamii, Ili tumsaidie asikumbane na vikwazo  tubadilike, tuondoe vikwazo ili tuweke mazingira jumuishi,” alisema  na kuongeza

“Shida kubwa ni hii hapa, ukiwa na jamii yenye mtazamo hasi, hii jamii itatengeneza sera mbovu, hizi sera ndiyo zinatengeneza mitazamo hasi. Tukiondoa mitazamo hasi dhidi ya watu wenye ulemavu, tutatengeneza jamii nzuri,” alisema Ernest.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa YoWDO, Rajab Mpilipili, amesema kundi hilo linakabiliwa na changamoto ya kuachwa katika fursa za maendeleo, hasa za kielimu na kiuchumi.

Amesema kwa kuwa jamii imeweka dhana potofu dhidi yao, kuwa hawawezi kufanya shughuli za kimaendeleo kutokana na ulemavu wao, kitu ambacho si kweli.

“Kumekuwa kunatolewa lugha mbaya juu ya watu wenye ulemavu, kitendo kinachopelekea wajione wanatengwa. Lugha nzuri itawafanya wenye ulemavu kujihisi wanathaminiwa na kuchukuliwa kama watu. Hii  Itasaidia kujenga jamii jumuishi,” amesema Mpilipili.

Mpilipili amesema watu wenye ulemavu wana haki ya kupata fursa za maendeleo sawa na watu wasiokuwa na ulemavu, ikiwemo ya kuajiriwa, kufanya biashara, kupata elimu na afya.