Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
RASMI uongozi wa klabu ya Yanga umetangaza kuachana na mabeki wao Kelvin Yondani na aliyekuwa nahodha msaidizi Juma Abdul
baada ya kushindwa kufikia makubaliano.
Hivi karibuni pande hizo mbili zilikuwa katika mazungumzo kuona ni namna gani wachezaji hao wataweza kusalia ndani ya kikosi msimu ujao baada ya mikataba yao kumalizika mwisho wa msimu huu.
Licha ya Yanga kutangaza kuwatema nyota 14 ambao hawakuridhishwa na viwango walivyovionesha lakini wachezaji hao walipewa nafasi ya pekee kutokana umuhimu wao.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa, katika mazungumzo hayo, viongozi wa Yanga walitaka wachezaji hao wasaini mikataba mipya bila kupewa fedha za usajili jambo ambalo waliligomea.
Imeelezwa, baada ya kuona ombi lao limekataliwa viongozi walikuja na ofa mpya lakini nayo haikuwaridhisha wachezaji hao na kuigomea na kuomba wakatafute changamoto katika klabu nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati ya ufundi Dominic Albinius, imesema pande hizo mbili zimeshindwa kukubaliana katika maslahi ya kuongeza mikataba.
“Klabu tumeona tuliweke hili wazi baada ya pande mbili kushindwa kukubaliana, wao kama wachezaji walikuja na ofa zao na sisi kama klabu tulikuja na mapendekezo yetu na baada ya mazungumzo tulishindwa kukubaliana,” amesema Albinius.
Hata hivyo Yanga imewatakia kila la kheri wachezaji hao wakongwe na ikiwashukuru kwa mchango wao wa kujituma na kuipa mafanikio Yanga katika kipindi ambacho wamefanya kazi.
“Tunawashukuru sana kwani wachezaji hawa wameitumikia klabu yetu muda mrefu na kwa mafanikio makubwa hivyo tunawatakia kila la kheri,” amesema Albinius.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania