March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yona adaiwa kumuua mpenzi wake kisha naye kujinyonga

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Wilbert Yona(34), mfanyakazi katika kiwanda cha Ziwa Steel na mkazi wa Kata ya Ihayabuyaga, wilayani Magu mkoani Mwanza,anadaiwa kumuua mpenzi wake aitwaye Marietha  Kalafala(33),pia ni mfanyakazi wa kiwanda hicho na mkazi wa Mwabuyi, kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kisha na yeye kujinyonga.

Akizungumza tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,amesema  tukio la vifo vya watu wawili vilivyotokea tarehe tofauti Desemba  27 na 28,2025.

Ambapo  tukio la mauaji ya Marietha Kalafala yaliripotiwa  Desemba 27,2025, majira ya 2 na dakika 15 usiku, katika Kitongoji cha Mwabuyi, Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu,ambaye 

aliuwawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni, mgongoni na kwenye paji la uso kisha wili wake kutupwa kwenye shamba la mahindi.

Mutafungwa amesema,baada ya ufuatiliaji ndipo Desemba  28,2025, majira ya 3.00 asubuhi, katika nyumba ya

kulala wageni itwayo Wema, iliyopo Kata ya Nyanguge Wilaya ya Magu, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa mmiliki wa nyumba hiyo kuwa kuna mteja wao amejiua kwa

kujinyonga kwenye chumba alichokuwa amekodi.

“Baada ya Askari Wetu kufika

kwenye nyumba hiyo mwili wa mtu huyo ulitambuliwa kuwa ni Wilbert  Yona,

aliyekuwa anatafutwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Marietha,”amesema Mutafungwa.

Amesema,miili ya marehemu imehifadhiwa katika kituo cha afya Lugeye, wilayani Magu, kwa

ajili ya uchunguzi wa kitaalamu na utakapokamilika miili itakabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi.

Hata hivyo ametaja  chanzo cha matukio haya ni wivu wa kimapenzi kwani

inadaiwa  Yona ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa akimtuhumu Marietha(marehemu) kuwa

na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengine.

Sanjari na hayo ametoa wito kwa wananchi hususani wapenzi na wana ndoa kuacha kujichukulia sheria mkononi wanapopata migogoro ya kimapenzi au ya kifamilia.

Na badala yake watafute msaada wa ushauri kupitia watu wanaowaamini, ustawi wa jamii, viongozi wa dini au vituo vya huduma ya kisaikolojia pale wanapopitia migogoro ya

kifamilia.