November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yashauriwa wakaguzi wenye ithibati ya umahiri kutumika kwenye miradi mikubwa

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

WAKAGUZI wenye ithibati ya umahiri nchini wametakiwa kutumika kipindi, ambacho Tanzania inatekeleza miradi mingi mikubwa ya ujenzi na maboresho ya miundombinu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza baada ya ujenzi kukamilika.

Ushauri huo umetolewa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Mwambole, wakati akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Dkt. Yusuf Ngenya kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ithibati (Accreditation) ambayo yaliadhimishwa na shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Ametoa mifano wa miradi hiyo inayohitaji wakaguzi wenye ithibati ya umahiri kuwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo inatumia umeme, ujenzi wa barabara za juu, ujenzi wa bomba la mafuta, ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka na mengine.

“Kuna mahitaji mbalimbali katika ujenzi wa miundombinu na majengo ambayo ni malighafi, bidhaa za ujenzi na wakaguzi wenye ithibati ya umahiri ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kujitokeza baada ya ujenzi kukamilika,” amesema Mwombole.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Mwambole, wakizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Dkt. Yusuf Ngenya kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ithibati (Accreditation) ambayo yaliadhimishwa na shirika hilo juzi jijini Dar es Salaam

Kutokana na umuhimu huo, ametoa wito kwa wadau wote kwenye mnyororo wa ugavi kutumia maabara zilizo na mifumo ya kimataifa ili kupata vipimo sahihi na vinavyokubalika kimataifa.

Ametolea mfano nchi zilizoendelea, akisema kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa malengo ya agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu hufanikiwa kwa kutumia viwango pamoja na huduma zinazotolewa na taasisi zenye ithibati ya umahiri kwenye upimaji, ugezi (Metrology), ukaguzi na uthibitishaji ubora.

“Katika nchi hizo ithibiti ya umahiri hutumika kama kigezo muhimu kuondoa vikwazo vya kibiashara na kukuza uchumi wa nchi, kukuza pato la taifa na kupunguza umasikini,” amesema Mwambole.

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujiuliza ni kwa jinsi wanaweza kutumia ithibati ya umahiri kutekeleza malengo ya agenda 2030 ya maendeleo endelevu.

Baadhi ya washiriki waliohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Ithibati Makao Makuu ya TBS, jijini Dar es Salaam juzi.

Kuhusu Ithibati, Mwambole alisema ni utambulisho wa kitaalam unaotolewa na taasisi na mamlaka za ithibati kudhibitisha umahiri katika kutoa huduma husika .

Kwa mujibu wa Mwambole kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni; “Ithibati kwa Utekelezaji ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (Support the Implementation of Sustainable development Goals).”
Sawa