January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

YARA yazindua mpango wa kugawa mbolea bure mkoani Kigoma

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Kigoma

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna Thobias Andengenye, amezindua mpango wa kugawa mbolea bure kwa wakulima wadogo unaoratibiwa na Kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania unaolenga uzalishaji wa mazao ya chakula hapa nchini.

Mpango huo unaojulikana kama Action Africa unalenga kugawa tani 12,500 za mbolea yenye thamani ya sh. bilioni 16.5 ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya mahindi na mpunga nchini.

Akizindua mpango huo jana, RC Andengenya amesema ujio wa mbolea hiyo kwa wakulima mkoani Kigoma utachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji chakula cha uhakika na kuongeza kipato kwa wakulima.

“Ni mpango mzuri na unaopaswa kupongezwa na kila mpenda maendeleo ya wakulima wa nchi hii kwani utaongeza upatikanaji wa chakula na pia kipato kwa mkulima mmoja mmoja hapa nchini na kwa Taifa kwa ujumla,” amesema.

Mbali ya kuimwaigia sifa kampuni ya Yara, RC Andengenye alitoa wito kwa kampuni zingine zinazojihusisisha na usambazaji wa zana na pembejeo za kilimo kuiga mfano wa Yara ili kuzidi kuimarisha sekta ya kilimo ambayo inaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 65.

Mpango huu uliopewa jina la Action Africa mbali ya kuwanufaisha wakulima kiuchumi na chakula, utaongeza uhakika wa malighafi kwa viwanda vyetu vya ndani ambapo Serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt. John Magufuli imekuwa ikitekeleza azma ya ujenzi wa viwanda.

“Nitoe wito kwa kampuni zingine kujitokeza na kusaidia wakulima kote nchini,” alisema. Aidha amewahimiza wakulima mkoani humo kujisajili ili waweze kunufaika na mpango huo.

“Hii ni fursa ya pekee kwa wakulima kujisajili ili waweze kunufaika na mbolea hii kwani mpango huo umekuja katika kipindi ambacho Serikali inatekeleza azma ya uchumi wa viwanda,” amesema Andengenye.

Kwa upande wake Meneja wa Biashara wa Yara Kanda ya Magharibi, Phillipo Mwakipesile aliipongeza Wizara ya kilimo kwa kuunga mkono jitihada zinafanywa na Yara za kuinua kilimo hapa nchini.

Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Kamishna Thobias Andengenye(kulia) akimkabidhi mbolea mmoja wa wakulima wadogo katika hafla ya uzinduzi wa mpango wa kugawa mbolea bure kwa wakulima ujuliakanao kama “Action Africa” unaoratibiwa na Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania. Kushoto ni Meneja biashara Kanda ya Magharibi wa YARA Tanzania, Phillipo Mwakipesile.

“Shukrani zetu ziende kwa wizara ya kilimo kwa namna ambavyo imekuwa ikituunga mkono kwa kipindi chote cha miaka 15

Naye Semeni Gumwa ambaye ni mnufaika wa mpango huo wa ugawaji mbolea bure alisema kwa miaka mingi wamelima bila kutumia mbolea na ujio wa mbolea hiyo kwao itakuwa ni fursa ya kuongeza uzalishaji.

Kwa miaka mingi hatujatumia mbolea katika uzalishaji wa mazao yetu hali ambayo ilitufanya tupate mavuno kidogo, tunaamini mpango huu wa mbolea bure ambao mimi kama sehemu ya wanufaika utatusaidia kuongeza uzalishaji na kukuza kipato chetu, alisema na kuwapongeza kampuni ya Yara kwa kurudisha faida wanayoipata kwa wakulima wa Tanzania.