Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
RAIS wa Yanga SC, Mhandisi Hersi Said na Viongozi wa timu timu hiyo wametembelea Hifadhi ya Taifa Arusha, Mei 18 mwaka huu kwa ajili ya kuona vivutio vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo.
Ugeni huo ulipokelewa na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Yustina Kiwango pamoja na viongozi mbalimbali waandamizi wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA).
Akizungumza mara baada ya kutembelea Hifadhi hiyo, Rais wa Yanga SC, Mhandisi Hersi amesema wamekwenda kutembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii.
“Sisi kama wanachama, viongozi na wapenzi wa Yanga SC, tumekuja hapa kuunga mkono jitihada za Rais za kuitangaza Tanzania yetu lakini pia tutatumia fursa hizi kutangaza kazi za Rais Nje ya Tanzania,” amesema Mhandisi Hersi.
Mhandisi Hersi amesema, amefurahi sana kutalii Hifadhi ya Taifa Arusha kwani amejionea madhari nzuri, wanyama na mimea ya kila aina pamoja na maporomoko ya maji.
Katika hatua nyingine Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki ameupongeza uongozi wa Yanga SC, ukiongozwa na Rais wa klabu hiyo, Mhandisi Hersi kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha.
Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Yustina Kiwango amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Klabu mbalimbali za michezo ambazo zimekuwa zikiiunga mkono adhma ya serikali ya Awamu ya sita katika kutangaza utalii wa nchi yetu.
Aidha, ametoa rai kwa wanachama kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kutangaza vivutio hivyo ndani na nje ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na kuvitembelea kwa wingi ili kuongeza pato la Taifa kupitia utalii wa ndani
Itakumbukwa Agosti 20, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alishiriki kurekodi Filamu mpya ya kuitangaza Tanzania iitwayo “Amazing Tanzania” ambayo imezinduliwa rasmi Mei 15 mwaka huu jijini Beijing, China.
Filamu hiyo imewashirikisha Marais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Mwinyi ambapo kupitia filamu hizo tumeshuhudia idadi kubwa ya wageni wa nje ya nchi pamoja na mwamko mkubwa wa watalii wa ndani wanaokwenda kuvitembelea vivutio vyetu na kuchangia pato la Taifa.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025