Na Penina Malundo,Timesmajira
JUZI, Januari 27 ilikuwa siku ya kwanza ya Mkutano wa siku mbili Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliomalizika jana.
Mkutano huo umeohudhuriwa na marais 24 wa Afrika ulianza jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).
Tanzania imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Africa Energy Summit) utakaofanyika jijini Dar es Salaam jana na leo.
Mkutano huu unaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Katika mkutano huu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye alikuwa mwenyeji wa Marais 24 kutoka nchi za Afrika, wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali 21, na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa sita, wakiwemo Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa Benki ya Afrika, na Rais wa Taasisi ya Rockefeller.
Aidha, washiriki 2,600 kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kushiriki katika tukio hili kubwa.
Marais na viongozi mbalimbali waliwasili nchini kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo.
Miongoni mwa marais hao ni pamoja na Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Tinubu alilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Mwingine ni Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania, Mohamed Ould Ghazouani.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mohamed Ould Ghazouani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, alipokelewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Festo Dugange,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Mwingine aliyeshiriki mkutano ni Rais wa Benki ya Dunia (WBG), Ajay Banga.
Banga aliwasili nchini Januari 26, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Banga alipokelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, .Dkt. Elsie Kanza, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Nathan Belete, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Rished Bade na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, alikutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki, Victoria Kwakwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia masuala ya Utawala, Anna Bjerde.
Mazungumzo hayo yalifanyika Jijini Dar es Salaam, Kando ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Nchemba aliwaeleza wageni wake kuwa Tanzania inahitaji zaidi ya dola za Marekani bilioni 12.9 zikiwemo dola za Marekani bilioni 4.04 kutoka Sekta Binafsi kwa ajili ya kuwekeza kwenye eneo la uzalishaji nishati nchini.
Katika kikao hicho kilichomhusisha pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Naibu wake, Amina Hamisi Shaaban, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza na viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, Dkt. Nchemba alieleza kuwa kiwango hicho cha fedha kitaiwezesha Tanzania kufikia uzalishaji wa nishati kwa asilimia 75 ifikapo Mwaka 2030 na kiwango cha asilimia 80 cha matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2034 na kutimiza lengo la kufikisha asilimia 65 ya nishati mchanganyiko itakayowezesha nchi kuzalisha Megawati 1,800 za umeme kwa njia ya umeme jua, upepo, joto ardhi na umeme wa kutumia nguvu ya maji.
Katika siku ya kwanza ya mkutano huo, Januari 27, 2025 Tanzania ilipongezwa kwa kufikisha nishati ya umeme hadi ngazi ya vijiji hali inayoendelea kuchochea maendeleo na ustawi kwa wananchi vijijini.
Pongezi hizo zilitolewa na Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) Dkt. Akinumwi Adesina, wakati wa mkutano wa nishati Afrika Missioni 300.
Alisema Tanzania ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine za Afrika kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu na miradi ya usambazaji.
Alisema Tanzania imeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuweza kusambaza umeme katika vijiji vyote 12,318.”
“Naomba nitumie fursa hii kumpongeza Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha wananchi wa Tanzania kufikiwa na nishati ya umeme katika vijiji vyote, jambo hili linastahili kupongezwa kutokana na umuhimu wa nishati hii katika maendeleo, ” alisema Dkt. Adesina.
Kuhusu mkutano wa nishati Afrika Dkt. Adesina alisema kuwa lengo ni kuwafikishia umeme watu Waafrika milioni 300 wanaoishi chini ya ukanda wa Jangwa la Sahara akisisitiza kuwa lengo hilo linakwenda kufanikiwa akisisitiza uwazi na uwajibikaji.
“Mkutano huu unalenga kuifungua Afrika kwenye eneo la nishati ya umeme, kuhakikisha wananchi katika nchi za Afrika wanaunganishwa na umeme”alisisitiza .
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Zambia, Dkt. Situmbeko Musokotwane, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiuzia umeme nchi yake kutokana na nchi hiyo kuwa na upungufu wa nishati hiyo.
“Tunashukuru Serikali ya Tanzania kwa kutuuzia umeme kwa sababu nchi yetu imekua na changamoto ya upungufu wa umeme”, alisema Dkt. Musokotwane
Mkutano wa nishati Afrika unafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, Tanzania ukiwakutanisha wakuu wa nchi za Afrika kwa lengo la kuwafikishia nishati ya umeme Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
Kwenye mkutano huo, ilielezwa kuwa ili Afrika ipate umeme wa uhakika, lazima kuwe na ushirikiano kati ya Serikali, mashirika ya fedha na asasi za kiraia kwa kuweka mipango itakayoleta matokeo ya uhakika.
Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja na Benki ya Dunia pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika siku ya kwanza ya mkutano huo.
Akizungumza katika mjadala ulioendeshwa na mwandishi wa habari wa CNN, Zain Asher, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina, alisema Bara la Afrika linapoteza kati ya asilimia 3 hadi 4 ya mapato yake ya ndani (GDP) kwa kukosa umeme.
Aidha, amesema zaidi ya watu milioni 600 hawana nishati ya umeme au nishati safi ya kupikia.
“Ninachotaka kusema ni kwamba tunamhitaji kila mtu, tunawahitaji wakuu wa nchi na Serikali, tunahitaji Benki ya Dunia na asasi za kiraia,” amesema Adesina.
Amesema kwa hali ya sasa, nchi za Afrika hazipaswi kufanya kazi kwa mazoea au kugawanyika.
“Hapa kuna Umoja wa Mataifa, Jumuiko la Nishati la Kimataifa, na Benki ya Kiislamu ya Maendeleo. Huu ni ubia mkubwa,” amesema na kuongeza;
“Wito wangu kwa viongozi wa nchi za Afrika watakaokutana kesho (leo) kuanisha miradi wanayoendesha katika nchi zao na kuongeza bajeti katika sekta ya nishati.
Lazima kuwe na mfumo wa ugavi na ununuzi wa nishati utakaoonyesha ugawaji wa nishati wa kikanda. Kitu cha pili tunachotegemea ni kwamba baada ya nchi 12 za Afrika kusaini makubaliano, zaidi ya watu milioni 140 wataanza kunufaika. “
Aliongeza kuwa; “Katika mkutano huu, suala si kuzungumza tu, mwisho wa yote, wananchi lazima wapate nishati.”
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga, amesema mkutano huo unatarajiwa kutoka na sera zitakazohakikisha watu milioni 600 wanafikiwa na umeme.
“Sera zinahitajika ili kufanya jambo hili liwe wazi, ili benki za biashara na sekta binafsi ziweke fedha zao na kupata matokeo yanayotabirika katika upatikanaji wa fedha,” alisema.
Aliongeza kuwa ili kuwe na matokeo yanayotabirika, miradi ya umeme haipaswi kuishia tu kuzalisha nishati, bali pia kuhakikisha umeme unawafikia wananchi.
Katika upatikanaji wa fedha za kuendesha miradi ya umeme, alisema wamelialika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kuziwezesha Serikali za Afrika kufanikisha miradi yao.
“Tumewaleta IMF hapa ili tuandae mifumo itakayofanya utoaji wa huduma hizi kuwa na tija zaidi. Kuna wabia waliojitokeza kuleta utabirika wa fedha kwa ajili ya miundombinu na ufadhili.
“Sehemu ya mwisho ni masoko ya nishati ya kikanda. Nadhani Tanzania imesema wana ubia na nchi nne na wanataka kuleta nchi ya tano.
Hili ni jambo tunalotaka lianze kutekelezwa barani Afrika,” amesema.
Kwa kupande wake Rais wa Rockefeller Foundation, Dk Rajiv Shah, alisema juhudi za kuongeza nishati Afrika zinapaswa kuanzia ndani ya bara hilo.
“Kwanza, kila mtu anafahamu kwamba ili tuwe na fursa ya kufanikiwa, jitihada hizo ni lazima ziongozwe kutoka Afrika. Idadi kubwa ya viongozi wa Afrika watakuja hapa na kutia saini makubaliano yatakayoleta mabadiliko ya sera na miundombinu. Nadhani haya ni mafanikio makubwa,” amesema. Dkt. Shah.
Amesema jambo la kutia moyo ni kuona tayari kuna wabia walioonesha nia ya kuwekeza Dola bilioni 43 za Marekani katika nishati tangu Mei 2024.
Dkt. Shah amesema katika mkutano huo kuna wawekezaji zaidi ya 200 waliokuja kuangalia fursa za kuwekeza katika sekta ya nishati.
“Hii inatupa matumaini kwamba Kusini mwa Jangwa la Sahara kutakuwa na juhudi za kusaidia uwekezaji ili kuimarisha taasisi za umma,” alisema.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko, amesema kuwa,Tanzania inachukulia mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika – Misheni 300 kama kichocheo cha utekelezaji wa Sera yake ya Taifa ya Nishati inayolenga kuendeleza nishati endelevu,uhifadhi na ufanisi.
Pia amesema maazimio ya nishati yaliyotayarishwa na nchi 14 yatakuwa ni maazimio ya majaribio ambayo yatakuwa yanatoa mfumo wa utekelezaji wa hatua zilizoratibiwa ili kufungua uwekezaji zaidi.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam,wakati akifungua Mkutano huo wa siku mbili ambao utatoa fursa ya kufanya majadiliano kati ya ngazi ya mawaziri na wadau wa masuala ya nishati na fedha na kesho.
Dkt. Biteko amesema kupitia mkutano huo utakuwa na manufaa kwa kupata umeme wa uhakika na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu upatikanaji wa nishati na ufumbuzi wake.
Amesema pamoja na maendeleo ya nishati yaliyopo nchini ,bado nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati kwani matarajio yake ni kukuza shughuli za kiuchumi hususan katika sekta za viwanda, madini na huduma za ukarimu jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa kimkakati zaidi katika sekta ya nishati.
“Sera hiyo pia inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati na kuongeza mchango wa nishati mbadala katika mchanganyiko wa uzalishaji ili kuimarisha upatikanaji, uhakika na usalama wa nishati,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa, Rais wa Tanzania, Dkt. Samia, amekuwa mstari wa mbele kukuza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani Afrika, jitihada ambazo zimeungwa mkono na mkakati wa kitaifa na kujumuishwa katika Azimio litakalotiwa saini katika mkutano huu, huku akitoa wito wa ahadi na ushirikiano zaidi katika kuboresha upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani mwetu.
Aidha, amesiisitiza kuwa ifikapo mwisho wa mwaka 2025, uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme utaongezeka hadi megawati 4,000, nishati inayotoka kwenye vyanzo safi na mbadala inavyonufaisha wakazi wa vijijini na mijini, huku miundombinu ya umeme ikifikia vijiji vyote 12,318 nchini.
Pia, amesema Tanzania inaimarisha muunganiko wa Afrika kwa kuwa na miundombinu ya umeme inayounganisha nchi za Kenya, Burundi, Rwanda, na Uganda, huku miundombinu ya kuunganisha Zambia ikiwa inaendelea.
Ametaja miongoni mwa mambo mengine yatakayofanyika katika mkutano huo kuwa ni kushirikishana uzoefu; kupata ahadi muhimu za kisiasa; kutumia ushirikiano ili kufungua uwekezaji wa sekta binafsi; kuanzisha ushirikiano wa kufadhili miundombinu ya nishati; na kukubaliana mfumo wa ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kiashiria cha Ufuatiliaji wa Maazimio ili kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Mkutano huo.
Alitoa rai kwa viongozi walioshiriki mkutano huo kutumia fursa hiyo kuhitimisha Maazimio yanayoendana na matarajio ya bara la Afrika ya nishati na kuimarisha ushirikiano unaohitajika katika kuyatekeleza.
“Ni matarajio yangu kwamba, mamlaka zinazohusika za nishati katika kila nchi ya majaribio zitajitahidi kuhakikisha maazimio ya nishati yanafanikishwa kupitia malengo na mipango ya hatua zinazolenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme, matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati mbadala na mchango wa mtaji wa sekta binafsi katika kufanikisha upatikanaji wa nishati”,alisisitiza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia(WB),Ajay Banga amesema kuwa bara la Afrika linaweza kubadilisha sura ya Afrika kwa kuwa na juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi Afrika ifikapo 2030
Nae Rais wa Benki ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina amelipongeza nchi ya Tanzania kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme kwa kuwafikishia nishati ya umeme wananchi katika vijijini vyote 12,318.
Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri wa Nishati, Viongozi wa Taasisi za Kimataifa za Kifedha, Wataalam na Wadau wa Mashirika ya Kiraia ambao watapata fursa ya kujadili na kukubaliana malengo, vipaumbele vya sera, suluhisho, na ahadi za jinsi ya kutekeleza Mpango wa Mission 300.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema hadi kufikia mwaka 2030 Watanzania wote watakuwa tayari wamefikiwa na umeme kutokana na mipango madhubuti iliyopangwa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Serikali unaoendelea katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).
Amesema kutoka na kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kufanikiwa, hivyo suala la umeme pia litafanikiwa kwa kila mtanzania.
Amesema mpaka kufikia mwaka 2030 Serikali ya Tanzania imekusudia kuhakikisha zaidi ya asilimia 75 ya watanzania watakuwa wamepata nishati safi ya kupikia.
Mramba amesema mkutano huu kufanyika hapa ni kama namna nyingine kutambua kazi kubwa ambayo nchi ya Tanzania imeweza kufanya.
”Ni uongozi wa Rais Samia katika nishati ya kupikia ambapo Rais Samia ametambulika Duniani kama ni Champion katika eneo hili la nishati ya kupikia na Tanzania tupo mstari wa mbele katika utekelezaji wa jambo hili.
”Ambapo sisi tumeonekana kuwa miongoni mwa nchi chache tumeonesha mfano ambapo Tanzania tayari imetengeneza mkakati wa utekelezaji wa nishati safi ya kupikia ambapo mkakati unaotoa miaka hadi 2034 kuweza kuwaamisha watanzania wote kutoka katika nishati isiyokuwa safi na kutumia nishati safi,”amesema.
Aidha amesema pia suala la Tanzania kuondokana na mgao wa umeme hili ni suala lingine ambalo Tanzania limetoa ujumbe kwa mataifa mengi ya Afrika juu ya uwezo na dhamira ya serikali ya Tanzania ya kuweza kuwafikishia wananchi wake umeme wa uhakika na kuondokana na matatizo ya changamoto nyingi za umeme.
”Mkutano huu unatuhakikishia mwaka 2030 Watanzania asilimia 100 wataweza kufikiwa na miundombinu ya umeme na wataweza kupata umeme na katika kipindi hicho watanzania ambao umeme umeingia katika nyumba zao wasiwe chini ya asilimia 75,pia katika kipindi hicho tunataka chini ya asilimia 75 wawe tayari wamepata nishati safi ya kupikia,”amesema.
Amesema mkutano huu utawaachia Watanzania wakiwa wametengeneza mahusiano makubwa na wadau mbalimbali sekta binafsi,washirika maendeleo,mabenki pamoja na watafiti.
Mramba amesema katika mpango huu serikali ya Tanzania imekusudia kuunganisha mita mpya milioni8.5 katika miaka mitano ijayo.
Hali ilivyokuwa
Katika siku mbili za mkutano huo Jiji la Dar es Salaam limekuwa kwenye mwonekano tofauti na ilivyozoeleka baada ya kubaki ‘jeupe’ kufuatia Mkutano huo uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).
Kufuatia mkutano huo mkubwa, wananchi mbalimbali wakiwemo waendeshaji wa vyombo vya usafiri vya bodaboda na bajaj walitii agizo la Serikali la kutoingia katikati ya mji kwa kipindi cha siku mbili za mkutano huo (ambao unaisha leo).
Aidha, watumishi wa umma Serikali iliwataka kufanyia kazi zao nyumbani, isipokuwa wale ambao mazingira ya kazi yao yanawahitaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jumapili na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, ilieleza kuwa wafanyakazi watakaotakiwa kufika maeneo yao ya kazi ni wale ambao mazingira ya kazi zao yanawahitaji kuwa katika vituo vya kazi kama vile watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji.
Licha ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupiga marufuku bodaboda na bajaji kuingia katikati ya jiji kutokana na mkutano wa kimataifa wa nishati, bajaji walitii agizo, lakini baadhi ya bodaboda walionekana wakikatisha maeneo ya katikati ya mji.
Januari 25, 2025, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu lilitangaza kufungwa kwa barabara tisa sambamba na barabara nyingine tisa kwa muda kupisha misafara ya viongozi mbalimbali wanaokuja kutoka nchi mbalimbali kuhudhuria mkutano wa nishati Afrika.
Aidha, Polisi iliagiza bajaji na bodaboda kutoingia katikati ya jiji katika kipindi chote ambacho mkutano huo unafanyika ambacho ni Januari 27 hadi Januari 28, 2025.
Gazeti hili lilishuhudia maeneo mbalimbali ilishuhudia bajaji zinazotoka maeneo ya Kimara na Mbezi zikiishia Jangwani, lakini bodaboda zilionekana zikikatiza mitaa kadhaa ya Posta na Kariakoo, ingawa
Bodaboda zilionekana zimebeba abiria waliokuwa wakiwashusha katika mitaa mbalimbali, ikiwemo ya Posta, ambapo baadhi ya barabara zilifungwa ili kupisha misafara ya marais wa mataifa ya Afrika wanaohudhuria mkutano.
Kikubwa ambacho kimeelezwa na abiria ambacho kiliwafanya hadi bodaboda kukaidi agizo a Polisi ni nauli, ambayo ilipanda hadi kufika sh. 17,000 kutoka Ubungo hadi Posta.
Wakati baadhi ya waendesha bodaboda walilalamikia hali ya biashara kutokana na zuio hilo, hali ilikuwa tofauti kwa waliokaidi agizo la Polisi ambapo walisikika wakisema jana ilikuwa siku ya kupga hela.
Hata hivyo, walikiri kuwa hali ya biashara sio nzuri hadi mkutano huo utakapomalizika leo. Wakati hayo yakiendelea maeneo mengi ikiwemo eneo la mkutano walitanda askari polisi waliokuwa wakifanya doria maeneo mbalimbali.
Katika viunga vya Posta Polisi wengine walikuwa kwenye magari kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, japo hali ilikuwa shwari.
Mabasi ya mwendokasi yalikuwa yakiendelea kutoa huduma ya usafiri kama kawaida, hasa kwa kwenda maeneo ya jiji kwa kuzingatia kwamba yana njia zake.
Teksi zinazoitwa na watenja kwa njia ya mtandao hazipatikani kirahisi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya abiria.
Wananchi wengi walisema abiria walikuwa wengi kuliko teksi, huku bajaj na pikipiki zikiwa zimepigwa kuingia mijini.
Baadhi ya bodaboda waliozungumza na gazeti hili walisema, Daud Michael, alisema hawaenda mjini katika siku hizi mbili za mkutano, kwani hawezi kupingana na kauli ya polisi.
Wakati hayo yakiendelea Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeongeza treni mbili za safari katikati ya jiji hilo ili kukidhi mahitaji ya usafiri.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Fredy Mwanjala, imezitaja treni hizo kuwa ni za Stesheni ya Kamata na Pugu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa treni hizo zitafanya safari zake saa 12:00 asubuhi kutoka Kamata na saa 12:05 jioni kwenda Pugu.
“Shirika la Reli Tanzania linapenda kuwatangazia kuwa, kutokana na kufungwa kwa barabara za kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kufuatia mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika, shirika limeongeza treni mbili za mjini kati ya Stesheni ya Kamata na Pugu jijini Dar es Salaam kwa tarehe 27 na 28, Januari 2025,” imeeleza taarifa hiyo.
Mwanjala alisema kuwa, pamoja na hatua hiyo, ratiba za awali za treni zitabaki kama kawaida.
Ameongeza kuwa treni hizo za ziada zitafanya kazi kwa saa zilizotajwa pekee, kipindi ambacho abiria wengi huenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia