May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WWF : Tuchukue hatua mabadiliko ya tabianchi

Na Penina Malundo 

SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) limeishauri Watanzania kuendelea kuchukua hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuhakikisha wanatunza mzingira ili kuweza kudhibiti kutokea kwa majanga mbalimbali.

Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi Mkaazi wa WWF Tanzania,  Dk. Amani Ngusaru wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano uliyoendeshwa kwa njia ya mtandao na kuhusisha nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kuendeleza kampeni ya ‘ Toa dakika 60 kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira’.

Dk. Ngusaru amesema Serikali imejitahidi na inaelewa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira lakini ni muhimu kuchukua hatua sasa ikiwemo ya upandaji wa miti ili kusaidia kukabiliana na  mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaonekana kukua kwa kasi kila kukicha.

“Tunapaswa kuendelea kuhimasisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, pamoja na jitihada mbalimbali tunazofanya bado hatujafikia lengo la kila mmoja kutambua umuhimu wa mazingira,  tunayosafari ndefu kwani mwamko kwa Serikali ni mkubwa ila kwa mtu mmoja mmoja bado.

“Mabadiliko ya tabianchi na mazingira yanapaswa kuwa jambo la kwanza kulizungumzia hapa nchini, WWF tutaendelea kuwaelimisha wananchi hasa kwa wazazi kuhakikisha wanawaeleza watoto wao umuhimu wa kusomea elimu ya mazingira kwani hivi vitamfanya kuwa mwanamazingira wa kisayansi,” amesema

Naye Meneja Mawasiliano WWF Tanzania, Joan Itanisa amesema katika kuhamasisha suala la uhifadhi wa mazingira,  wanatarajia kupanda miti 5000 ndani ya wiki moja katika maeneo mbalimbali likiwemo la Pugu Mnadani jijini Dar es Salaam.

Itanisa amesema upandaji wa miti hiyo utafanyika Machi 25, mwaka huu katika eneo hilo ambalo ni chazo cha mto Msimbazi ambao unajulikana na wakazi wengi wa Dar es Salaam.

“Tunawahamasisha na watu wengine ambao hawataweza kuunga na sisi siku hiyo, nao kutumia dakika zao 60 kufanya jambo fulani linaohusu mazingira lengo ni kusaidia uhamasishaji wa uhifadhi wa mazingira,” amesema Itanisa

Aidha amesema mwaka huu wametambulisha kampeni hiyo mpya ya toa dakika 60 kwaajili ya kuhifadhi mazingira ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii walau mara moja kwa mwaka kutoa muda huo kuwekeza katika masuala ya mazingira.Â