Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza
Shirika la WoteSawa limewapatia mafunzo ya kutengeneza taulo za kike za kufua (sodo) na elimu ya afya ya uzazi wasichana na wanawake 15 kutoka Mwanza na Ngara,ili kuhamasisha suala la hedhi salama.
Hedhi salama kwa watoto wa kike na wanawake ikiwemo wanaofanya kazi za nyumbani huchangia kuwa na familia salama na kusaidia wasichana kutimiza ndoto zao ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kutumia wakati wa hedhi pamoja na elimu sahihi juu ya suala zima la hedhi na matumizi ya vifaa.
Akizungumza na TimesMajira Online jijini Mwanza makao makuu ya shirika , Ofisa Msimamizi wa Makao na Uwezeshaji wa shirika la WoteSawa linalojishughulisha na kutetea haki za mabinti wafanyakazi wa nyumbani Demitila Faustine, ameeleza kuwa mafunzo hayo ya siku nane yametolewa na shirika hilo chini ya ufadhili wa KULCZYK Foundation yenye lengo la kuhamasisha hedhi salama,kwa watoto wa kike na wanawake yalioanza Machi 1hadi Machi 8, mwaka huu jijini Mwanza.
Demitila ameeleza kuwa,suala la hedhi salama kwa wasichana na wanawake ni changamoto hivyo wamewapatia elimu ya afya ya uzazi pamoja na mafunzo ya kutengeneza taulo za kike za kufua,ili kuhamasisha suala la hedhi salama.
“Baada ya mafunzo hayo wanufaika watatengeneza na kuzalisha taulo za kike 1,000 za kufua kwa ajili ya kuuza kwenye jamji kwa gharama nafuu ambayo na wasichana na wanawake wengine wataweza kumudu,”ameeleza Demitila.
Mkufunzi wa taulo za kike za kufua(sodo),kutoka shirika la WoteSawa Vicky Edward, ameeleza kuwa lengo la mafunzo ni kuwapatia ujuzi na uelewa wa namna ya kutumia taulo za kike ambazo zitapatikana kwa haraka ambapo jumla ya washiriki 15 wamepatiwa mafunzo hayo.
Pamoja na kuwajengea uwezo wa kuona kuwa kuna fursa katika suala zima la hedhi ambayo ni utengenezaji wa taulo za kike za sodo kwani akisha fahamu hatoishia tu yeye kuvaa binafsi bali anaweza kutumia kama fursa ya kujiingizia kipato kwa kuuza.
“Tunawajengea uwezo pia wa kufanya biashara kupitia pedi za sodo ambazo zina uwanda mpana na watumiaji wake ni wengi hapa duniani kwani suala la hedhi ni endelevu la kila siku ambalo mwanamke au binti lazima atakutana na hali hiyo kila mwezi,”ameeleza Vicky.
Pia ameeleza kuwa pedi ni sehemu muhimu katika maisha ya mwanamke na wamekuja na taulo za kike za kufua kwa sababu zinatumika zaidi ya miezi 12, hivyo itasaidia kupunguza gharama na ukizingatia wengi wao kipato chao ni duni.
Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo,Deisa Elia, ameeleza awali alipokuwa akifanya kazi za nyumbani kabla ya kuokolewa na WoteSawa mwajiri wake alikuwa hajawai kumfundisha jinsia ya matumizi sahihi ya taulo za kike pia waajiri wengi hawawapatii vifaa vya kujistiri wakati wa hedhi.
Ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo amefahamu namna ya kushona taulo za kike za kufua hivyo anatarajia kuwafundisha wasichana wengine ili na wao waweze kufundisha wengine na hatimaye waweze kumaliza changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kujistiri wakati wa hedhi na kwa gharama nafuu kwa wote bila kujali hali ya uchumi pamoja na jinsi ya kuzitumia.
“Nalishukuru wote sawa kwa mafunzo haya kwani taulo za kike hizi za sodo tutatumia zaidi ya mwaka na tutaweza kutengeneza wenyewe nyumbani endapo tutakuwa na vifaa pia yatatusaidia kiuchumi kwa kupunguza bajeti ya kila mwezi ya kununua taulo za kike.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa,ili kukabiliana na changamoto ya vifaa vya kujistiri wakati wa hedhi kwa wanawake na wasichana sanjari na kujikimu kiuchumi ameiomba serikali na wadau watoe mafunzo zaidi kwa wasichana juu ya utengenezaji wa taulo za kike za kufua huku ikihakikisha hupatikanaji wa malighafi za kutengezea taulo hizo zinapatikana kwa urahisi na gharama nafuu.
“Serikali itilie mkazo katika suala la hedhi salama kwa kuhakikisha wasichana na wanawake wanapata mafunzo ya kutengeneza taulo za kike huku na wao waende kuwafundisha wengine,nitakaporejeshwa nyumbani nitaenda kuendeleza ujuzi huu kwa sababu una wasaidia wasichana wengi kuondokana na utegemezi wa taulo hizo na uchumi pia,”.
Neema Ishengoma, ameeleza kuwa suala la upatikanaji wa taulo za kike ni changamoto hivyo serikali iwaangalie watoto wa kike kwa jicho la ziada kwa kuhakikisha taulo hizo zinapatika kwa gharama nafuu.
Ambapo ameeleza kuwa wakitoa elimu sahihi kwa jamii wao ambao wamepata mafunzo hayo itasaidia hupatikanaji wa taulo za kike kwa urahisi endapo watashikwa mkono kufanya kwa vitendo kile walichofundishwa.
“Nalishukuru shirika la WoteSawa kwa kitupatia mafunzo hayo ambayo yametujengea uwezo juu ya hedhi salama,na namna ya kuweza kukabiliana na changamoto ya uhaba wa taulo za kike ambazo tutaweza kuzalisha wenyewe na kufundisha wengine,hivyo serikali ituwezeshe mitaji ili tuzalishe kwa wingi pedi hizi ambazo zinatumika kwa muda mrefu na kutupunguzia gharama,”ameeleza Neema.
Annaflora Laurent,ameeleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kuwa na ujuzi hivyo matarajio yake ni kuanza shughuli za uzalishaji wa taulo za kike hivyo serikali iendelee kutoa elimu zaidi kwa waajiri ili wafanyakazi wa nyumbani waweze kujifunza na kuwa na ujuzi ambao utawasaidia kujikwamua kiuchumi.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi