September 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WMA:Dira 2050 itajengwa kwa vipimo sahihi

Na Zena Mohamed,TimesMajira Online,Dodoma

WAKALA wa Vipimo Nchini (WMA) umesema utaendelea kuwa chombo muhimu katika kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa kuhakikisha kilo moja inakuwa kilo moja, lita moja inakuwa lita moja na mita moja inakuwa mita moja, hatua inayolenga kujenga uaminifu katika biashara, kulinda mlaji na mtoa huduma pamoja na kusaidia Serikali kupata mapato yake kwa usahihi kupitia vipimo vilivyohakikiwa.

Wakala huo umesema katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 utaendelea kuhakikisha matumizi ya vipimo sahihi ili kujenga Tanzania yenye uchumi imara, jumuishi na shindani.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo Septemba 18,2026 na Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA,Alban Kihulla,  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Amesema WMA itaendelea kuwa chombo muhimu katika kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akishukuru vyombo vyote vya habari kwa mchango wao mkubwa katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi.

Kutokana na hayo WMA imewaonya wafanyabiashara wanaotumia vipimo visivyo sahihi au kuuza bidhaa kwa vipimo visivyokidhi viwango kwamba wanakabiliwa na adhabu kali kwa mujibu wa sheria, ikiwemo faini na kifungo.

Kwa mujibu wa Kihulla, mtuhumiwa anayekubali kosa anaweza kutozwa faini ya Shilingi 100,000 hadi 20,000,000 kwa kosa moja, huku anayekataa kosa na kupatikana na hatia akipelekwa Mahakamani na kutozwa faini ya Shilingi laki tatu hadi milioni 50, au faini na kifungo kisichozidi miaka miwili.

Amesema kwa mkosaji wa mara kwa mara, faini inaweza kuwa kati ya Shilingi 500,000 na milioni 100 kwa kosa moja, hatua inayolenga kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia matumizi ya vipimo sahihi na kulinda haki za walaji.

Kihulla amewataka wakulima kuachana na matumizi ya magunia, madebe, makopo, mafungu na vipimo vingine visivyo rasmi katika biashara ya mazao, akisisitiza matumizi ya mizani kwa kuwa kilo ndiyo kipimo kinachotambulika katika biashara kote duniani.

Amesema matumizi ya vipimo visivyo rasmi yanaweza kusababisha kutokuwepo kwa usawa katika biashara, hivyo wananchi wanapaswa kudai kupimiwa bidhaa kwa mizani ili kuhakikisha wanapata kiasi halisi wanacholipia.

“Madebe, makopo, visado na mafungu siyo vipimo, wafanyabiashara tumieni mizani,” amesisitiza Kihulla, akieleza kuwa WMA inahakikisha kilo moja inakuwa kilo moja na vipimo vyote vinazingatia viwango vinavyotambulika.

Aidha, amesema WMA haisimamii vipimo vya bidhaa pekee, bali inahakikisha usahihi wa vipimo katika sekta mbalimbali kwa mujibu wa sheria za kitaifa, kikanda na kimataifa.

Kihulla ametoa mfano wa sekta ya afya, ambako vipimo vya uzito vimekuwa vikihakikiwa ili kuhakikisha mgonjwa anapata uzito halisi, jambo linalomsaidia daktari kuamua kiwango sahihi cha dawa kinacholingana na uzito wa mgonjwa.

Amewataka wananchi kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya matumizi ya vipimo visivyo sahihi kwa kutoa taarifa wanapobaini au kuhisi kuwa vipimo vinavyotumika au walivyopimiwa si sahihi.