Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAIMU Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Albogast Kajungu amefanya ziara ya kushtukiza katika mashamba ya wakulima mbalimbali eneo la Mang’ola wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha na kuridhishwa na namna wakulima hao wanavyozingatia matumizi ya vipimo sahihi.
Akiongoza Timu ya Wataalamu wa WMA katika zoezi hilo, Agosti 9, mwaka huu, Kajungu amesema lengo ni kujiridhisha ikiwa wananchi wanazingatia elimu inayotolewa na Wakala wa Vipimo kuhusu matumizi ya vipimo sahihi ili kuzilinda pande zote yaani wakulima, wafanya biashara na walaji.
Katika ziara hiyo, Timu hiyo ya Wataalamu wa WMA walihakiki uzito wa mazao aina ya vitunguu yaliyofungashwa katika vifungashio vya aina mbalimbali tayari kwa kuuzwa pamoja na kuzungumza na wakulima, wafanyabiashara na wasafirishaji wa mazao hayo.
“Niwapongeze sana kwa kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi maana katika mazao yote yaliyofungashwa ambayo tumepima, hakuna yaliyozidi uzito unaoelekezwa kisheria. Nawasihi muendelee hivyo kwani kila upande utapata faida stahiki,” amesema Kajungu.
Akifafanua zaidi kuhusu maelekezo ya kisheria kwa uzito wa mazao ya shamba yaliyofungashwa, Kajungu amesema mkulima yuko huru kufungasha kwa kutumia aina yoyote ya kifungashio isipokuwa azingatie uzito wake usizidi kilo 100.
Ametoa ufafanuzi huo kutokana na uelewa tofauti kwa baadhi ya watu wanaotafsiri kuwa sheria inakataza kufungasha mazao kwa kuongeza kishungi katika vifungashio.
“Niendelee kuwaelimisha na kuwaelewesha kuwa tafsiri sahihi ya lumbesa siyo kishungi bali ni uzito uliozidi kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa, Na katika hili niseme wazi huwezi kuthibitisha lumbesa kwa macho, ni lazima upime kujiridhisha kuwa mazao yaliyofungashwa yamezidi kilo 100,” amesisitiza Kajungu.
Katika hatua nyingine, Kajungu ameendelea kutoa ushauri kwa Halmashauri zote nchini kutumia mizani kupima mazao yaliyofungashwa ili kuondoa utata na manung’uniko yanayojitokeza kwa baadhi ya wakulima na wafanyabiashara kwamba wanatozwa faini kwa mazao yaliyofungashwa na kuwa na kishungi yakitafsiriwa kama lumbesa.
“Mwarobaini wa changamoto hiyo ni kutumia mizani kama sheria inavyoelekeza na siyo kutizama kwa macho.”
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima na wafanyabiashara wa vitunguu katika eneo la Mang’ola wamekiri kunufaika zaidi kwa kila upande baada ya kuanza kuzingatia elimu ya vipimo sahihi waliyopatiwa na Serikali kupitia Wakala wa Vipimo.
Marieta Tlemai, mkulima wa vitunguu, kwa niaba ya wenzake, ametoa pongezi kwa Serikali kupitia Wakala wa Vipimo kwa kuwajali wakulima na kuweka sheria ya ufungashaji mazao inayolenga kulinda maslahi yao.
Awali, Timu hiyo ya Wataalamu kutoka WMA, ilitembelea Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu ili kueleza dhamira ya ziara yao na kupokelewa na Katibu Tawala, Dkt. Lameck Karanga ambaye aliwahakikishia kuwa Ofisi yake inaunga mkono jitihada za kutokomeza lumbesa ili kulinda maslahi ya wananchi wake ambao wengi hujishughulisha na kilimo cha vitunguu.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi