Na Penina Malundo, Timesmajira
Wakala wa Vipimo (WMA) umetekeleza Mpango Kazi wake wa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa asilimia 96 ya malengo iliyojiwekea, kufikia mwezi Mei mwaka huu.
Hayo yalibainishwa Juni 13, 2025 na Mtaalamu wa Uchumi kutoka Kitengo cha Mipango cha WMA, Benjamin Nkwera wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa kipindi husika kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi lililoketi katika Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Katika taarifa yake, Mtaalamu huyo wa Uchumi alieleza kwamba katika kipindi husika, mikoa 25 imefanikiwa kufikia malengo kwa asilimia 100 huku mikoa minne ikifikia malengo kwa zaidi ya asilimia 90 na miwili ikiwa na asilimia chini ya 80.
Miongoni mwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa Makao Makuu ya Wakala jijini Dodoma, ununuzi wa magari na vitendea kazi vingine, pamoja na kuajiri wataalamu katika kada mbalimbali.
Aidha, ameeleza kuwa Wakala imefanikiwa kuhakiki vipimo 1,191,833 kati ya 1,238,391 sawa na asilimia 96.24 ya lengo.
“Kati ya vipimo vilivyokaguliwa na kuhakikiwa, vipimo 16,210 vilirekebishwa na 1,161 vilikataliwa,” alidadavua Nkwera.
Ameongeza kuwa katika kipindi husika, Wakala imefanya kaguzi 4,231 kati ya 3,667 zilizopangwa, sawa na asilimia 115.38.
Kazi nyingine iliyotekelezwa ni ukaguzi na ufuatiliaji wa vipimo vinavyotumika kwenye ushushaji wa mafuta jamii ya petroli pamoja na mafuta ya kula ambapo alisema kuwa jumla ya Meli 161 zilizoingia nchini zenye jumla ya lita 9,955,936,919 zilikaguliwa.
Akizungumza na wajumbe wa Baraza hilo, Mwenyekiti wake ambaye ni Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla amewaasa kufanya kazi kwa bidii, upendo na kushikamana huku wakijiepusha na vitendo vya rushwa ili kuendelea kupata matokeo chanya kwa faida ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), Mkoa wa Dar es Salaam, Sara Rwezaula ameipongeza ushirikiano uliopo baina ya Uongozi wa Wakala na wafanyakazi ambao alisema ndiyo hasa ulioleta chachu ya matokeo chanya ya utendaji wa WMA.
“Nampongeza na kumshukuru Mtendaji Mkuu na Menejimenti yote kwa kuendelea kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Baraza la Wafanyakazi,” amesisitiza.
Kikao hicho cha 36 cha Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Vipimo kilitanguliwa na kikao cha Kamati Tendaji kilichofanyika siku moja kabla, Juni 12, 2025.
Wakala wa Vipimo ni moja ya Wakala na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Jukumu lake kuu ni kumlinda mlaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kupitia matumizi ya vipimo sahihi na kwa usahihi.
More Stories
Kamishna wa umeme na nishati jadidifu afanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme jijini Dar
Majaliwa:Wanufaikaji Mikopo ya Elimu ya Juu kuongezeka
Diwani Zingiziwa aeleza mikakati yake ya maendeleo