Na Mwandishi Wetu, Mngeta
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi, inafuatilia hukumu ya kesi ya uharibifu wa ekari 24 za shamba la mpunga, inayomkabili, mfugaji Kapimilo Kini, inayotarajiwa kutolewa kesho.
Hukumu ya kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, inatarajiwa kutolewa kesho na Mahakama ya Mwanzo ya Mngeta wilayani Mlimba, mkoani Morogoro.
Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mussa Kulita wa Mahakama ya Mwanzo Mngeta, Kapimilo anayemiliki zaidi ya ng’ombe 10,000, anadaiwa kufanya uharibifu wa ekari 24 za mpunga, kwa kuachia mifugo yake kula ndani ya shamba la Rashid Shaibu, kinyume cha sheria.
Taarifa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Waziri Ashatu Kijaji, zilieleza kuwa taarifa za kesi hiyo walizipata kupitia vyombo vya habari wiki jana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wizara inaamini kuwa endapo haki itatendeka katika kesi za migogoro ya wakulima na wafugaji, zitapungua.Hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima ni uvunjaji wa sheria, na Serikali haitavumilia, akitaka wafugaji wafuge kulingana na maeneo ya malisho.
Majaliwa amesema hayo karibuni akizungumza na wananchi kwenye vijiji vya Nanjaru na Mkaranga vya kata ya Nambilanje na kijiji cha Nankonjera, kata ya Namichiga akikagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa Ruangwa, Lindi.
“Kilimo ni maisha, ni biashara, ni fedha na vivyo hivyo ufugaji ni maisha, biashara na fedha, hivyo kila mkulima alime kulingana na ukubwa wa eneo lake na mfugaji afuge mifugo kilingana na ukubwa wa eneo lake na malisho.
“Sisi sote ni Watanzania na tunataka utajiri. Wakulima na wafugaji waheshimiane, kwani wote ni Watanzania,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema migogoro ya wakulima na wafugaji haina tija na Serikali haitaki kuona ikiendelea na hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine, hivyo kila mmoja awe na mpango kazi usioathiri upande wowote.
Kadhalika Waziri Mkuu amewataka watendaji wa vijiji kabla hawajagawa maeneo kwa wafugaji, wahakikishe idadi ya mifugo waliyonayo na washirikishe serikali za vijiji na wananchi.
“Wafugaji badilikeni, fugeni kisasa, msione fahari kuwa na idadi kubwa ya mifugo mnayoshindwa kuihudumia. Fugeni mifugo michache mtakayohudumia vizuri na kuiuza kwa gharama kubwa,” ameshauri.
Ameagiza Wizara kukaa na wizara za kisekta, ili kusaidia wakulima na wafugaji kuondokana na migogoro, kwani mingi hutokana na kutotengwa maeneo halisi ya wafugaji na hali hiyo imesababisha malalamiko katika maeneo mbalimbali nchini.
KESI YA KAPIMILO
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, tukio hilo lilitokea Juni 23 jioni eneo la Chita kwa ng’ombe wa Kapimilo kudaiwa kula mimea kwenye shamba la Shaibu na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.Hukumu ya kesi hiyo inayovuta hisia za wengi katika kijiji cha Chita, imekuja baada ya Mahakama hiyo, kumaliza kusikiliza mashahidi wa mashitaka na utetezi.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako