November 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Mifugo na Uvuvi, TADB wawezesha ufugaji wa Samaki

Na Mwandiahi Wetu,TimesMajira

SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewezesha vijana 167 kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara kupata mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.3 kwa ajili ya kuendeleza ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT Uvuvi).

Akizungumza katika uzinduzi wa uvunaji samaki uliofanyika Nyegezi jijini Mwanza, Meneja wa Usimamizi wa Miradi wa TADB, Eveline Shayo, amesema uwezeshaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kutoa zaidi ya Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya uzalishaji na biashara.

Amesema katika kutekeleza programu hiyo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inashirikiana na Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) pamoja na TADB, ambapo benki hiyo imepokea Shilingi bilioni 7.9 kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa BBT Uvuvi unaolenga kuwawezesha vijana katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, kilimo cha mwani, unenepeshaji kaa na ufugaji wa majongoo bahari.

Shayo amesema katika eneo la Nyegezi jijini Mwanza, jumla ya vikundi 12 vyenye vizimba 80 vimewezeshwa kwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.06, inayojumuisha upatikanaji wa vizimba, vifaranga vya samaki, chakula cha samaki pamoja na fedha za kujikimu kwa wanufaika kwa kipindi cha miezi saba.

Ameongeza kuwa TADB imekuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu fedha za mikopo pamoja na kutoa ushauri wa masuala ya kifedha kwa vijana wanufaika ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu

Katika uzinduzi huo, zoezi la uvunaji samaki limefanyika kwa vikundi vitatu vyenye jumla ya vizimba 20 vilivyopandikizwa samaki mwezi Aprili mwaka huu, vikiwa na mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 516.

Kupitia uvunaji huo, vikundi hivyo vinatarajia kupata wastani wa tani saba hadi tisa za samaki kwa kila kizimba, huku programu ya BBT Uvuvi ikitarajia kuwafikia vijana zaidi ya 500 na kuendelea kupanua wigo wa uwezeshaji katika mikoa mingine, ikiwemo Geita.